Banda la kuku wa kienyeji


Banda bora la kuku linatakiwa kuwa kama ifuatavyo:
Liwe jengo imara

  • Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
  • Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
  • Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
  • Jengo mara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.
Liwe rahisi kusafisha
  • Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
  • Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
  • Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au maranda ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira yako.
  • Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika katika banda.
  • Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa hudhibitiwa.
Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.

Ufugaji wa nusu huria
Liweze kuingiza hewa na mwanga wa kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa safi na kutoka ndani yake hubaki kavu. Harufu mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa safi. Hii husaidia pia kudhibiti kuzaliana kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo hudhibiti magonjwa.Banda liwe na nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo: Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha kuku wanne wanaotaga au kuku 8 wa nyama. Nafasi ya mita mraba 1 inatosha vifaranga 16 hadi kufikia umri wa majuma manne.

Lisiwe na joto sana au baridi sana: Panda miti ya kuzunguka banda lako ili eneo liwe na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina joto kubwa kwa vipindi virefu paa la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu mzunguko zaidi wa hewa na joto la paa ( kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku.

Joto kwenye banda linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji aangalie aweke idadi ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.

Paa lifunike ukuta kwa sehemu kubwa
Liwe imara na lisilovuja. Waweza kutumia mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na upatikanaji wa vifaa vya kuezekea.Wakati wa kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali liwe na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia mvua kuingia ndani kama ni ya upepo ( angalia mchoro hapa chini).

Vifaa vinavyohitajika katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya banda na ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu viwe katika banda:

Kinywesheo cha kujitengenezea
Kuna njia nyingi za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji ya kuku ya kunywa.

  • Aina ya mojawapo unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo hiyo pande nne kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha. Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
  • Au waweza kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafiliwe kirahisi.
  • Vifaa maalum vya kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.

Kilishio
Tabia hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.Vyombo hivi ni muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula. Unapotengeneza kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza au kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini.

Unaweza kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.



Muunganiko wa viota
Pia ipo aina nyingine inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota kimoja kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota kimoja( angalia picha hapa chini).Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30 na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota.Zipo aina tofauti za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni ya kutagia kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa sentimita 30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe wazi ila sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao (angalia kielelezo). Weka idadi ya viota inayotosheleza kuku ulio nao.


Viota vinatakiwa kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza husaidia kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa mahali ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu itakayorahisisha usafishaji wa kiota chenyewe.