1.0 UTANGULIZI:
Jina la kitaalamu ni Zingiber officinale
Tangawizi ni aina ya zao la kiungo ambalo sehemu inayotumika ni tunguu
(rhizome) ambalo huonekana kama mizizi ya mmea. Asili ya zao hili ni maeneo ya
kitropiki ya bara la Asia na hasa katika nchi za India na China. Zao hili
linazalishwa kwa wingi kutoka katika nchi ya Jamaica. Hapa nchini zao hili
hulimwa katika mikoa ya Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Kilimanjaro.
Tangawizi hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na
kuchangamsha katika vinywaji (kama soda, juisi, vilevi n.k) na vyakula
mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga, achari n.k. Hutumika
pia katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za
meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi n.k. pia hutumika katika vipodozi
kama poda n.k).
2.0 AINA ZA TANGAWIZI
Hakuna uthibitisho wa aina za tangawizi ambazo hulimwa hapa nchini ila
kuna dalili ya kuwa na aina za White Africa (Jamaica) na Cochin (flint); hii
huwa na tunguu ngumu zenye nyuzi.
3.0 TABIA YA MMEA
Tangawizi ni mmea
unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu ya ardhi. Jamaica
ina rangi hafifu ya kahawia na tunguu fupi wakati Cochin ina
tunguu fupi zaidi lenye ngozi ya rangi iliyo
kati ya kijivu na nyekundu. Mmea una urefu wa futi mbili na majani yake ni
membamba marefu ambayo hufa kila mwaka yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua
ya mmea huu yana rangi nyeupe au manjano.
4.0 HALI YA HEWA NA UDONGO
Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa
bahari hadi mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha
mm.1,200-1,800 na joto la wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25. Hustawi vema
katika udongo tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.
5.0 UPANDAJI
Zao la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu vyenye
kichipukizi kizuri angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sm.2.5-5.
Wakati mwingine, vichipukizi vinavyopatikana katika kumenya tangawizi huweza
kuhifadhiwa na kutumika kwa kupanda. Kiasi cha kilo 840-1700 cha vipande vya
tunguu huweza kutumika kwa kupanda katika hekta moja.
Nafasi inayotumika kupanda ni kati ya sentimita.23-30 kwa 15-23 na kina
cha sentimita.5-10 na mara nyingi hupandwa katika matuta. Baadhi ya mazao
huweza kupandwa katika shamba la tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa si
lazima kivuli kiwepo. Inashauriwa kumwagilia maji endapo mvua inakosekana. Wiki
1-2 kabla ya kupanda weka mbolea ya samadi au mboji kiasi cha tani 25-30 kwa
hekta na kwa kukuzia weka kiasi cha NPK kwa uwiano wa kilo 36:36:80. Tandaza
nyasi shambani kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapokosekana.
Palizi hufanywa mara magugu yanapoota, dawa ya kuua magugu, kama
simazine hutumika.
7.0 Magonjwa na wadudu:
• Madoa ya majani yanayosababishwa na viini
vya magonjwa viitwavyo Colletotrichum zingiberis na Phyllosticta zingiberi.
• Kuoza kwa tunguu; kunasababishwa na viini
viitwavyo Pithium spp
• Mizizi fundo; inasababishwa na Meloidegyne
spp.
8.0 UVUNAJI
Tangawizi huweza kuwa tayari kwa kuvuna kati ya miezi 9-10 baada ya
kupanda, wakati majani yake yanapogeuka rangi kuwa njano na mashina kusinyaa.
Tangawizi inayohitajika kwa kuhifadhi kwenye kemikali (preserved ginger in
brine) huvunwa kabla haijakomaa kabisa, wakati ile iliyokomaa kabisa huwa kali
zaidi na huwa na nyuzi hivyo hufaa kwa kukausha na kusaga. Mavuno hutofautiana
kulinganana na huduma ya zao, mavuno yanaweza kuwa kiasi cha tani 20-30 cha
tangawizi mbichi huweza kupatikana.
9.0 USINDIKAJI
Tangawizi ikisindikwa utapata unga, mafuta maalum (essential oils) n.k.
Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa, kukatwa na kukaushwa juani au
mara nyingine huchovywa katika maji yaliyochemka kwanza na ndipo kukaushwa au
hukamuliwa mafuta.
Pia tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa
zimechanganywa na sukari na/au chumvi. Hata hivyo tangawizi ina Kiasi cha
mafuta cha 16.0-18.0%.
10.0 SOKO LA TANGAWIZI
Soko la tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi kikubwa kinauzwa
nchini. Bei yake ni kati sh. 300-1,500/- kutegemeana na msimu.
11.0 GHARAMA ZA UZALISHAJI NA MAPATO
GHARAMA YA HEKTA MOJA:
Mbegu Tshs. 240,000/-
Vibarua 250,000/-
Mbolea(mboji/samadi) 150,000/-
Jumla 640,000/-
MAPATO:
Kilo 20,000 X300 =6,000,000/-