Makala hii inalenga zaidi wale ambao wanafikiria kuwa wajasiriamali. Iwapo wewe ni mjasiriamali tayari basi makala hii itakuwa kama ukumbusho kwako wa vitu vya muhimu unavyotakiwa kufanya. Lengo ya haya yote ni kupunguza ugumu wa safari iliyo mbele yako kuelekea mafanikio. Moja kwa moja twende katika vitu hivi kama ifuatavyo.
1. JIFUNZE KUJIPA MOYO
Maisha ya ujasiriamali sio ya mtelemko. Unaweza kukutana na changamoto mbalimbali ukiwa unaelekea mafanikio. Wengi hukata tamaa njiani kwa sababu ya hili. Wale wasiokata tamaa ni wale wenye uwezo wa kujisukuma kusonga mbele hata kama kila kitu kinaenda vibaya.
Ni uwezo wa kujipa tumaini la mafanikio hata kama hujaambulia kitu siku hiyo katika biashara yako. Ni uwezo wa kuinuka baada ya kuanguka mara moja baada ya ingine. Ni uwezo wa kujivuta na kusogea hatua moja zaidi mbele hata kama unajihisi kushindwa kabisa. Jifunze hili na utafikia ndoto zako bila kujali nini kinakukabili.
2. JIFUNZE KUWEKA AKIBA
Siku za hivi karibuni nilikuwa nasoma makala flani mtandaoni nanukuu “Laki tano ni pesa ya kununulia Heinken 100 katika viwanja vya bata, lakini hiyohiyo laki tano ukiitunza unaweza kwenda kuwekeza katika kilimo ikakuingizia pesa zaidi”. Nadhani sentensi hiyo hapo juu inaongelea vizuri moja kati ya faida ya kutunza pesa.
Moja kati ya maswali ambayo naulizwa sana ni jinsi ya kupata mtaji ili kuanzisha biashara. Ukitazama wafanyabiashara wengi wakubwa leo walianza na mitaji waliyoipata baada ya kutunza pesa za mishahara au biashara nyingine ndogondogo. Zaidi ya hapo hujui kesho ikoje. Kuwa na kiasi kizuri cha pesa cha akiba kunaweza kuokoa biashara yako wakati wa misukosuko.
3. JIFUNZE KUUZA (MBINU ZA MAUZO)
Huwezi kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio kama hujui mbinu za mauzo. Napenda nilirudie hili kwa herufi kubwa. HUWEZI KUWA MJASIRIAMALI MWENYE MAFANIKIO KAMA HUJUI MBINU ZA MAUZO.
Kuanzia kujua jinsi ya kupokea wateja hadi jinsi ya kuagana nao wakishanunua bidhaa kutoka kwako, mbinu za mauzo hutumika. Hili ni jambo ambalo inabidi uanze kulielewa mapema kama unataka kuwa mjasiriamali. Unaweza kuanza kidogokidogo kwa kuongea na watu walio wajasiriamali au kwa kufanya uchunguzi mtaani kwako na katika mtandao.
4. ANZA KUJENGA MTANDAO WA WATU
Asilimia 80 ya kazi kubwakubwa nilizowahi kupata katika maisha yangu zimetokana na mtandao wa watu nilioujenga. Marafiki zangu, walimu wangu, wateja wangu wameleta kwangu tenda ambazo sikuwa naweza kupata kwa kawaida.
Si hivyo tu, pale nilipokuwa napata changamoto flani, ni watu hawahawa walio katika mtandao wangu ndio walinisaidia kuzipita. Na hii ndio hali ya dunia ilivyo kwa sasa. Mtu akiwa na fursa mara nyingi atampa fursa hiyo mtu katika mtandao wake. Hii ni dunia nzima. Kazi ni kwako kuwa sehemu ya mtandao wa watu wanaoweza kukusaidia kufika mbali zaidi katika biashara yako.
5. FANYA KAZI KWA MASAA MAREFU (Masaa 80 hadi 100 kwa wiki)
Kama umeajiriwa ni rahisi sana kujisahau na kudhani hali itaendelea kuwa hivyo pale utapojikita katika ujasiriamali moja kwa moja. Ujasiriamali hauna masaa maalumu ya kazi. Unaweza ukapiga kazi siku saba za wiki. Hususani katika kipindi cha mwanzo, ni muhimu sana kutumia muda mwingi uwezavyo katika biashara yako ili kuhakikisha inakua vizuri.
Kujiandaa na hili ni vema ukaanza kujizoesha kufanya kazi kwa masaa marefu. Kama umeajiriwa basi fanya kazi overtime. Kama ni mwanafunzi basi tafuta kaajira cha ziada kama hali inaruhusu au ongeza muda zaidi katika masomo yako. Hii ni ili kujenga zaidi uwezo wa kufanya kazi kwa bidii ili utakapojikita katika ujasiriamali usikate tamaa kirahisi baada ya kuona masaa ya kazi ni mengi.
6. JIFUNZE KUFANYA UTAFITI NA JIFUNZE HARAKA
Katika miaka ya hivi karibuni kuna usemi wa kiingereza umekuwa maarufu sana. Msemo huu unasema “Information is Power” yani “Kujua jambo ni Nguvu”. Kila siku utasikia watu waliofanikiwa wakiongelea jinsi walivyoona fursa ya kuanzisha biashara flani.
Unadhani walionaje hiyo fursa? Utafiti. Utasikia wengine wakisema baada ya muda flani wakaongeza bidhaa kutokana na uhitaji wa bidhaa hiyo. Unadhani walionaje uhitaji huo? Utafiti. Utasikia wakisema wamefanikiwa kuongeza mauzo baada ya kutumia mbinu flani ya kujitangaza. Wamejuaje kujitangaza kwa mbinu husika kunaweza kuwasaidia? Utafiti.
Kuwa mtafiti ujue mambo ya muhimu yanayoendelea katika eneo la ujasiriamali na hutakosa fursa za kuingiza kipato milele.
7. TAMBUA NI VITU GANI UNAWEZA VIZURI NA CHUNGUZA AINA MBALIMBALI ZA BIASHARA
Huwezi kila kitu. Kuna baadhi ya vitu una vipaji navyo au umekuwa mtaalamu baada ya kujifunza kwa muda mrefu. Ukimchukua mchezaji mpira wa kimataifa ukamuambia akashindane kuogelea uwezekano mkubwa atakuwa kituko.
Tambua uwezo wako ni nini na ukishafanya hivyo unaweza kujenga biashara yako kwa kuzingatia hili ili uwe na uwezekano mkubwa zaidi wa kufanikiwa. Lakini pia chunguza aina mbalimbali za biashara uone wapi patakufaa. Usiseme unataka kuwa mkulima kama hauko tayari kujifunza kuanzia bei za pembejeo hadi jinsi ya kupanda.
Chagua biashara ya kufanya kutokana na utayari wako wa kuifanya biashara hiyo kwa bidii ili ufikie mafanikio. Ukienda kichwakichwa utaishia kuambulia hasara tu.
8. JIWEKE KATIKA HALI ZA KUFA NA KUPONA
Vuta pumzi kwanza. Ninapomaanisha kufa kupona simaanishi usimame katikati ya barabara ukiomba magari yasimame kabla ya kukugonga. La hasha. Maana yangu hapa ni kuwa jitahidi kujiweka katika kazi au majukumu ambayo yanahitaji kukamilika ndani ya muda maalumu ili kila kitu kiende sawa.
Ukifanya hili utakuwa unajijengea uwezo wa kuhimili mikikimikiki katika biashara. Hii ni kwa sababu mara nyingi katika ujasiriamali unahitaji kupangilia vizuri vitu vyako ili ufanikiwe lakini pia uwe na uwezo wa kufanya kazi kubwa ndani ya muda mdogo.
Kwa kuwa tayari ulishakuwa na majukumu kama haya ukiwa kazini au kwingineko (mfano shuleni) basi kuna uwezekano mkubwa utafikia mafanikio haraka zaidi.
MWISHO
Ni vema kuzingatia haya mambo kama unataka kuwa mjasiriamali au hata kama wewe ni mjasiriamali tayari. Lakini pia nataka utambue jambo flani hapo juu. Utaona katika mambo nane yaliyotajwa hapo juu, mambo manne (4) yanaanza na neno JIFUNZE. Hii inamaanisha kuwa kujifunza ni nusu ya unalotakiwa kufanya ili ufanikiwe katika ujasiriamali. Si mtaji, si madili na wala si ndumba bali ni KUJIFUNZA.
TEMBELEA TUVOTI YETU HII. KUPATA ELIMU ZAIDI.