SWALI: Tathmini ni nini?
Fafanua kwa dhima dhana ya tathmini.
Wataalamu mbalimbali
wametoa ufafanuzi kuhusu dhana ya tathmini na wamefafanua kama ifuatavyo;
WEU, (2005), Tathmini ni
upimaji wenye nia ya kuelezea iwapo malengo yametimia katika kiwango fulani.
WU, (2014), tathmini ni
utaratibu wa kuchunguza na kupima hali halisi kwa lengo la kupata data
zitakazomwezesha mwalimu au mtahini kufanya maamuzi yanayohusu urekebishaji au
uboreshaji wa mambo mbalimbali.
Wataalamu wote
wanaelekeana kukubaliana kuwa tathmini ni utaratibu wa kupima hali halisi kwa
lengo la kupata taarifa zitakazomwezesha kufanya maamuzi yanayohusu
urekebishaji au uboreshaji wa mambo mbalimbali.
Kwa mujibu wa WEU, (2005),Kuna
aina nne za tathmini ambazo hutumika zaidi katika elimu ,nazo ni; Tathmini ya
awali, ambayo hutumika kupima wahusika
wanaotarajia kujiunga na kozi au mafunzo fulani kama wanayo maarifa na
stadi kiasi cha kutosha kuwawezesha
kuanza masomo mapya bila matatizo .mfano shule binafsi hutoa mtihani wa kuanza masomo ya kidato cha
kwanza.
Tathmini endelevu (formative
evaluation), hufanyika wakati wote katika kipindi cha mafunzo ,ili kujua
mafanikio wakati wa ufundishaji au utekelezaji
wa mpango wa elimu. Taarifa zinazopatikana husaidia katika kutatua matatizo yanayobainika
kuwepo.
Tathmini ya kudodosa
(diagonistic evaluation) hufanyika katika kutafuta chanzo cha tatizo ambalo
njia mbalimbali za kutatua tatizo zimetumika bila kupata mafanikio ya
kuridhisha. Mfano mwalimu darasani anaweza kumfanya mwanafunzi wake mmoja
kushindwa kutofautisha nomino na viwakilishi
licha ya kutumia mbinu mbalimbali katika kufundisha. Hivyo mwalimu
anaweza kufanya tathmini ya kudodosa
huenda mwanafunzi huyo akawa na matatizo ya kiafya ,kijamii au kisaikolojia Baada ya kugundua
tatizo alilonalo utaratibu wa kumwondolea tatizo hilo huandaliwa.
Tathmini tamati
(summative evaluation) ,hufanyika mwishoni mwa kozi au mafunzo, pia mwishoni
mwa kipindi cha jaribio au mradi wa elimu. Matokeo ya tathmini hii huonesha
kiasi cha mafanikio yaliyofikiwa kufuatana na malengo yaliyowekwa awali. Pia huonesha matatizo yaliyojitokeza .vilevile
matokeo ya tathmini hii hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wa kuendelea na
mafunzo ya juu ,kwa mfano waliohitimu
darasa la saba kujiunga na kidato cha kwanza .Aidha tathmini hii hutumika
katika kuamua kama malengo ya somo au kozi ni muafaka na vilevile kama
ufundishaji ni bora au ni duni.
Kwa mujibu wa kamusi ya
karne ya 21: Dhima ni wajibu mkubwa, madaraka au jukumu. Hivyo kwa mujibu wa
WEU, (2005) dhima ya dhana ya tathmini ya elimu nchini Tanzania ni kupima hali
halisi ili kuweza kufanya maamuzi yatakayohusu urekebishaji au uboreshaji wa
hali iliyopo kulingana na malengo yaliyowekwa. Dhima ya kufanya tathmini katika
elimu ni pamoja na;
Kugundua matatizo waliyonayo
wanafunzi yanayoathiri ujifunzaji wao. katika harakati za kujifunza wanafunzi
hukabiliwa na matatizo mbalimbali yanayoathiri ujifunzaji wao, matatizo hayo yaweza kusababishwa na
mazingira, urithi ,magonjwa ama hali ya kiuchumi ya familia. Hivyo ni lazima
mwalimu kufanya tathmini ya hali ya ujifunzaji kwa wanafunzi ili kuweza
kugundua changamoto wanazokabiliana wanafunzi na kuzitafutia ufumbuzi ili
malengo ya ujifunzaji yaweze kufikiwa.
Kuwapa wanafunzi matokeo
ya maendeleo yao ili waweze kutambua kama ni mazuri au mabaya. katika mchakato
wa kujifunza ni lazima kufanyika upimaji ili kujua mafanikio ya ujifunzaji na
ufundishaji, hivyo matokeo ya upimaji hutoa tathmini ya maendeleo ya mwanafunzi
kama ni mazuri ili aweze kuongeza jitihada za kufanya vizuri zaidi a kama ni si
mazuri kuweza kuchochea ari katika kujifunza ili kupata matokeo mazuri.
Kuwapatia walimu taarifa
kuhusu ufanisi wa njia na vifaa vya kufundishia na kujifunzia .tathmini
husaidia kuleta mrejesho kwa walimu kuhusu mafanikio ya njia ,mbinu na zana
walizotumia katika mchakato wa ufundishaji
na ujifunzaji kwani matokeo
yanapokuwa mazuri huonesha kufanikiwa kwa mbinu zilizotumika hivyo kuweza
kuziboresha zaidi na yakiwa mabaya
humaanisha kushindwa kwa mbinu zilizotumika hivyo kumfanya mwalimu kutafakari
mbinu nyingine mpya za kufundishia ili kuweza kupata mafanikio mazuri.
Kuwapatia wazazi ,walezi
na wadau wengine wa elimu maendeleo ya wanafunzi .Tathmini hutumika kutoa
taarifa kwa wadau mbalimbali wa elimu katika ngazi ya shule ,jamii hadi taifa
hivyo kutoa taswira ya maendeleo ya shule kama ni nzuri huweza kupongezwa na kumotishwa,
kama ni mbaya huweza kuchunguzwa ili kubaini sababu za kufanya vibaya na kuchukua hatua za
kuboresha ili kufanya vizuri na kufikia malengo ya utoaji elimu. vilevile
maendeleo mazuri huweza kuifanya jamii kuvutiwa kufanya shughuli za maendeleo
ya shule kama vile ujenzi wa miundombinu na kuchangia ununuzi wa samani pamoja
na kutoa zawadi. Aidha wazazi wa wanafunzi wanaofanya vibaya huweza
kushirikiana na walimu katika kutafutia ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili
wanafunzi hao.
Kujua ufanisi wa mpango
wa elimu uliopo ili kuweza kurekebisha matatizo yaliyopo ,na kama ni mradi wa
majaribio kuweza kuamua kutokuendelezwa au kutekelezwa nchi nzima. Ipo mipango mbalimbali
yenye lengo la kuendeleza sekta ya elimu mfano MMES, MMEM na mingineyo ,hivyo
tathmini ni kitu muhimu katika kupima kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mpango na
kuchukua hatua za kuendelea ,kuboresha ama kubadilisha kulingana na kufanikiwa
au kutofanikiwa kwa malengo.
Kuhakikisha kwamba
rasilimali zilizowekwa katika mpango hazipotei au kutumika vibaya .ili mpango
wowote uweze kutekelezwa ni lazima kuwe na rasilimali mbalimbali kama vile
rasilimali watu, rasilimali fedha, rasilimali muda na rasilimali miundombinu. Rasilimali
watu ni wadau wote watakaoshiriki kwa namna yoyote ile kufanikisha utekelezaji
wa mradi au mpango uliowekwa. Rasilimali fedha ni kiasi cha fedha kilichopangwa
katika kugharamia mambo mbalimbali wakati wa mradi au mpango uliowekwa. Rasilimali
muda ni wakati uliopangwa katika kutekeleza mradi au mpango husika hadi kufikia
malengo yaliyokusudiwa.
Rasilimali miundombinu ni
jumla ya vitu vilivyopangwa kutumika katika kufanikisha utekelezaji wa mradi au
mpango fulani uliowekwa.
Hivyo tathmini hutumika
kuonesha ni kwa namna gani rasilimali zilizopangwa zimetumika kwa makusudio
yaliyowekwa ama hazikutumika ipasavyo na kuchukua hatua stahiki. Tathmini ni
muhimu sana kwa kila jambo tulifanyalo kwani hupelekea kujua mafanikio ya
malengo yaliyotarajiwa na kuweza kuchukua hatua za kuboresha, kurekebisha
kasoro zilizojitokeza ama kuondoa
kabisa kama mpango umeonekana kutoleta
tija.
SWALI: Jadili aina za tathmini kwa mifano huku
ukihusianisha na uhalisia ulivyo.
WU, (2014).
Tathmini ni utaratibu wa kupima na kuchunguza hali halisi kwa lengo la kupata
data zitakazomwezesha mwalimu au mtahini kufanya maamuzi sahihi yanayohusu
urekebishaji au uboreshaji wa mambo mbalimbali katika elimu.
Luwingu,
anafafanua kuwa, tathmini ni tendo la kutafuta ni kwa kiasi gani mwanafunzi
amepaa maarifa au stadi zilizofundishwa kufuatana na malengo ya ufundishaji wa
mada za somo yaliyopo kwenye muhtasari. Upimaji katika elimu pia hujumuisha
mwenendo wa tabia ya mwanafunzi na uwezo wake wa kufanya mambo mbalimbali.
Rossi &
Freeman, (1993). Tathmini ni mchakato wa kupima wenye malengo ya kuangalia
utaratibu, utekelezaji, maboresho au matokeo ya programu.
Kwa ujumla,
tathmini ni kitendo cha kutaka kujua kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mpango
fulani ulioandaliwa mfano tathmini ya elimu kwa lengo la kufanya uboreshaji wa
mambo mbalimbali katika elimu. Zifuatazo ni aina za tathmini.
Tathmini ya
awali. Tathmini hii pia hutambulika kama tathmini ya kupima uwezo wa kumudu
masomo mapya. Katika aina hii ya tathmini wahusika hupimwa kama wanayo
maarifa na stadi kiasi cha kutosha
kuwawezesha kuanza masomo mapya bila matatizo. Mfano shule binafsi hutoa
mtihani wa kuanza masomo ya kidato cha kwanza (WEU, 2005).
Tathmini
endelevu. Tathmini ya aina hii hufanywa au hufanyika wakati wote katika kipindi
chote cha mafunzo. Madhumuni yake ni kuweza kujua mafanikio na matatizo
yanayotokea wakati wa ufundishaji au utekelezaji wa mpango wa elimu. Taarifa
zinazopatikana husaidia katika kutatua matatizo yanayobainika wakati huo. Mfano
wakati wa ufundishaji ndani ya kipindi cha dakika 40, 60 au 80. Pia tathmini
hii inaweza kufanywa kwa kumtathmini mwanafunzi wakati wote wa kozi hiyo (WEU,
2005).
Tathmini
gunduzi. Aina hii ya tathmini pia huitwa tathmini ya kudodosa. Katika
ufundishaji, tathmini ya aina hii hufanyika katika kutafuta chanzo cha tatizo
ambalo njia mbalimbali za kulitatua zimetumika bila ya kupata mafanikio ya
kuridhisha. Mfano, mwalimu darasani anaweza kushindwa kumfanya mwanafunzi wake
mmoja aelewe aina za maneno pamoja na kutunga sentensi mbalimbali.
Katika hali
kama hii mwalimu anaweza kufanya tathmini ya kudodosa kwa mwanafunzi huyo.
Inawezekana mwanafunzi huyo ana matatizo ya kiafya, kijamii au kisaikolojia.
Baada ya kugundua tatizo alilonalo mwanafunzi huyo, ndipo utaratibu maalumu wa
kumwondolea tatizo hilo huandaliwa na kutekelezwa (WEU, 2005).
Tathmini ya
tamati. Aina hii ya tathmini pia hutambulika kama tathmini ya mwisho. Tathmini
hii hufanyika mwishoni mwa kozi au mafunzo au mwishoni mwa kipindi cha jaribio
au mradi wa elimu. Matokeo ya tathmini hii huonesha kiasi cha mafanikio
yaliyofikiwa kufuatana na malengo ya yaliyokuwa yamewekwa awali. Pia huonesha
matatizo yaliyojitokeza.
Katika
ufundishaji, matokeo ya tathmini hii huweza kutumika katika uchaguzi wa
wanafunzi wa kuendelea na mafunzo ya juu, kwa mfano kidato cha kwanza au
kujiunga na mafunzo ya kozi mbalimbali. Tathmini tamati pia hutumika kuamua
kama malengo ya somo au kozi ni muafaka na vilevile kama ufundishaji ni bora au
ni duni (WEU, 2005).
Walimu wa
somo la lugha ya Kiswahili wazingatie
aina zote (nne) za upimaji ambazo ni tathmini ya awali, tathmini
endelevu, tathmini gunduzi na tathmini ya mwisho ili kuona kama maarifa na
stadi wanazofundisha zinafikiwa au hazifikiwi kulingana na malengo ya elimu
yaliyowekwa.
SWALI: Kuandaa mazoezi ni moja ya upimaji,
eleza dhana ya upimaji inavyotumika katika elimu pamoja na kanuni zinazotakiwa
kufuatwa katika uandaaji wa mazoezi na mitihani.
Dhana
ya upimaji
KEH,
(2013). Upimaji ni kazi
ya kutambua tabia za kitu kwa umakinifu. Mara nyingi tabia hizi zinatazamiwa
kwa njia ya makadirio lakini kila kadirio hutegemeana na mtu mwenyewe
anayekadiria. Pale ambako watu mbalimbali wanataka kulinganisha vitu viwili
wakati wanatofautiana katika makadirio yao upimaji unaweza kuamua juu ya
ukubwa, uzito na tabia nyingine.
WEU, (2005). Katika elimu upimaji ni
tendo la kutafuta ni kwa kiasi gani mwanafunzi amepata maarifa au stadi
zilifundishwa kufuatana na malengo ya ufundishaji wa mada za somo zilizopo
kwenye muhtasari. Upimaji katika elimu unajumuisha mwenendo na tabia ya
mwanafunzi na uwezo wake wa kufanya mambo mbalimbali.
Kwa ujumla, upimaji katika elimu ni tendo la kutafuta ni kwa kiasi gani
mwanafunzi amepata maarifa au stadi zilizofundishwa kufuatana na malengo ya
ufundishaji na mada za somo yaliyopo katika muhtasari. Katika elimu upimaji
hujumuisha mambo mbalimbali kama taaluma, tabia na mwenendo, na uwezo wa
mwanafunzi katika kumudu stadi mbalimbali. Upimaji katika elimu haupo kwa
wanafunzi tu na hata kwa walimu. Mwalimu
hupimwa kuonesha uwezo wake katika elimu, ambapo ni vile anavyopima na matokeo
anayoyapata kama wanafunzi wamefaulu au la. Hivyo ndivyo mwalimu anavyopimwa.
Dhana ya mtihani
Mtihani ni
njia moja wapo ya upimaji ambayo mtu anapimwa kutokana na alichokisoma au
alichofundishwa ili atambuliwe kwamba alielewa au hakuelewa. Au ni kipimo cha maisha kutokana na ulichojifunza. Katika shule mwanafunzi hupimwa na walimu wake juu ya kile walichomfundisha ili
kumjua kama anaelewa au haelewi. Mitihani yaweza kuwa migumu au rahisi kutokana
na mwanafunzi mwenyewe: kama huwa hajisomei ataiona migumu na kama anajisomea
ataiona rahisi hata kama mwalimu alitunga migumu kiasi gani (KEH, 2017).
Mazoezi na mitihani hizi ni zana za
upimaji katika elimu, ambazo mtu hupimwa kutokana na alichokisoma au
alichofundishwa ili atambuliwe kama alielewa au hakuelewa. Kuna namna
mbalimbali za kutoa mazoezi kama vile; unapofundisha kwa kutumia njia
shirikishi, mazoezi hutolewa kwa kutumia maswali na majibu. Pia mazoezi
yanatolewa kwa njia ya kuandika. Inahimizwa zoezi la kuandika litolewe kila
unapomaliza dhana, mada kuu/ndogo. Pia ni vema likasahihishwa ili kupata
mweleko wa wanafunzi wako. Mitihani hutolewa mwisho wa muhula au kozi au
mafunzo (WEU, 2005)
Mitihani hutumika kuonesha maendeleo
ya mwanafunzi kwa kila somo kwa kulinganisha na alama za wanafunzi wengine.
Matokeo ya mtihani hutumwa kwa wazazi au walezi wa wanafunzi ili kuweza kujua
maendeleo ya mwanafunzi wao. Pia kuna mitihani mikuu inayofanyika katika shule
zetu nchini kama vile mtihani wa kidato cha sita, kidato cha nne, kidato cha
pili, darasa la saba na darasa la nne ambayo ni mitihani ya kitaifa (WEU,
2005).
Kanuni
zinazotakiwa kufuatwa katika uandaaji wa mazoezi na mitihani.
Kufuata misingi ya utungaji wa
maswali ya aina mbalimbali. Mtihani unaunganisha aina mbalimbali za maswali
kama maswali ya kuchagua jibu sahihi, maswali y kweli na si kweli, maswali ya
kuoanisha, maswali ya kuandika jibu moja fupi na maswali y insha. Aina hizi
zote kila moja ina misingi yake ya kuzingatia wakati wa utungaji. Hivyo katika
kutunga mtihani ni vizuri kuzingatia misingi ya kila aina ya maswali
utakayohitaji yawepo katika mtihani wako (WEU, 2005).
Maswali ya maumbo mbalimbali
yaambatane na vielelezo. Maswali yote ambayo yanahitaji michoro inafaa
iambatane hapohapo katika swali na visiwe katika kurasa nyingine. Vielelezo
hivyo ni kama vile picha, ramani na michoro. Vielelezo hivyo visiambatane na
vitu vingine visivyohitajika kupimwa katika mtihani (WEU, 2005).
Ni vizuri kutoa mfano wa tukio au
tatizo na kisha kuuliza swali linalomtaka mwanafunzi aweze kutabiri matokeo au
aeleze njia/mbinu za kutatua tatizo. Katika mtihani yapo maswali yanayolenga
kutabiri matokeo ya jambo fulani katika maisha linaloendana na somo au kunaweza
kukawa na tatizo fulani katika jamii hivyo humtaka mtahiniwa kuonesha njia au
mbinu za kutatua tatizo hilo hivyo ni vyema ukatoa mfano katika muundo wa swali
lako (WEU, 2005).
Maswali yalingane na hali halisi ya
mambo au mazingira. Katika utungaji wa maswali ya mtihani inafaa maswali
yaendane na mambo halisi yaliyopo katika jamii na mazingira halisi. Haifai hata
kidogo kutunga maswali kutokana na mambo ya kufikiria, yasiyo ya kawaida au
yasiyoweza kutekelezeka. Mtahiniwa huandaliwa kupambana na changamoto
zinazoikabili jamii. Hivyo ni lazima apimwe katika masuala yanayohusiana na
jamii (WEU, 2005).
Kupanga maswali. Msingi huu unajikita
katika kupanga mtihani kwa mtiririko unakubalika. Kupima kuanzia na maswali
rahisi yakifuatiwa na maswali magumu. Aidha mtihani nzuri ni ule unaoanza na
maswali yanayopima makazi ya chini ya upimaji kukimaliziwa na maswali
yanayopima makazi ya juu ya upimaji (WEU, 2005).
Misingi mingine ni:
- · Orodhesha vipengele vya kupima
- · Aina ya maswali
- · Kila kipengele cha upimaji lazima oneshe mambo anayokusudia kupima
- · Mtiririko na lugha iliyotumika
- · Liwe na kiwango cha upimaji
- · Kuandaa majibu
- · Kuonesha mgawanyo wa alama kwa kila swali.
- · Vipengele vya upimaji ambavyo vinapatikana katika jedwali la upimaji
Hivyo katika uwandaji wa maswali ya
mazoezi na mitihani ni vizuri kuzingatia misingi hii ili kufanya mazoezi na
mitihani kuwa bora.
SWALI: fafanua
sifa za mtihani mwafaka kisha eleza vitu muhimu vya kuzingatia kabla ya kufanya
mtihani.
Mitihani ni upimaji unaotolewa baada ya mwanafunzi
kumaliza ngazi fulani ya elimu. Mwanafunzi hufanya mtihani ili aweze kuingia
darasa lingine au aingie ngazi nyingine ya elimu( elimu ya msingi kuingia elimu
ya sekondari). Mtihani hutolewa katika muda maalumu na muda huo hauna budi
kujulikana kwa mtahiniwa. Mtihani hutolewa na chombo maalumu kilicho wekwa na
umma kwa madhumuni yao (TET,2002).
Mtihani ni njia ambayo mtu anapimwa kutokana na alicho
soma au alicho fundishwa ili atambuliwe kwamba alielewa au hakuelewa. Pia ni
kipimo cha maisha kulingana ulicho fundishwa
kutoka kwa jumuiya unayoishi nayo (WEU,1999).
Mtihani mwafaka ni mtihani anao tunga tena mwalimu na
kuwapa wanafunzi wake baada ya mtihani wa kwanza kutokidhi vigezo. Hivyo huenda
wanafunzi wamefaulu kupita kiasi yaani mtihani kuwa rahisi sana au wanafunzi
kufeli kupita kiasi yaani mtihani kuwa mgumu kupita kiasi, maana yake mtihani
umeshindwa kupima makazi ya juu na makazi ya chini (TET, 2002)
Mtihani mwafaka
huwa na sifa mbalimbali na hizi zifuatazo ni baadhi ya sifa za mtihani mwafaka
Mtihani mwafaka uzingatie ngazi ya walengwa na uwezo
wao, mwalimu unapo tunga mtihani unatakiwa uzingatie umri, ngazi ya wanafunzi
waliyofikia na uwezo wao wa kupambanua na kujibu maswali, unapo kuwa na mtihani
ambao haukuzingatia kigezo hiki itakuwa ngumu sana kumpima mwanafunzi na kuona
kama ulichofundisha amekielewa au hakuelewa kwa kuwa umetunga bila kuangalia
uwezo wao na ngazi yao kielimu, ila ukifuata kigezo hicho utakuwa na nafasi ya
kumpima mwanafunzi na kujua uwezo wake katika kujifunza (TET,2002).
Pia uwe na lugha rahisi inayo eleweka kwa watahiniwa,
mwalimu unapotunga mtihani unatakiwa kutumia lugha rahisi ambayo watahiniwa
wataielewa kwa urahisi kinyume na hapo watahiniwa watashindwa kuelewa maswali
na hatimaye kushindwa kujibu mtihani au kujibu tofauti na ulivyo tarajia
kwakuwa watahiniwa walishindwa kuelewa lugha uliyo tumia katika maswali na
kuwafanya washindwe kujibu vizuri, yawezekana maswali hayo wanayajua na ulisha
wafundisha darasani na kufanyia mazoezi lakini ukatumia maneno magumu ambayo
watahiniwa hawayajui na hujawahi kuwafundisha maneno hayo hivyo itapelekea
watahiniwa hao kushindwa kujibu mtihani huo (TET,2002).
Vilevile uwe na mtiririko mzuri wa maswali kuanzia
maswali rahisi kwenda maswali magumu, mwalimu unapotunga mtihani usio zingatia
kigezo hiki unaweza kushindwa kufanikisha upimaji wako kwakuwa mwanafunzi anapo
jibu mtihani akianza na kukutana na maswali magumu atakata tamaa na kuona
mtihani huo mgumu bila kujua kuwa kuna maswali yapo ambayo anaweza kuyapata,
kwakuwa ameanza na kuona maswali magumu hivyo mtahiniwa anaweza kushindwa
kujiamini na hatimaye akakata tamaa ya kujibu mtihani huo na kufeli kabisa
mtihani huo (TET,2002).
Aidha uzingatie
muda wa kuanza na muda wa kumaliza mtihani huo, mwalimu unapo wapima wanafunzi
kwa kutumia mtihani lazima mtihani wako uoneshe wazi kuwa utaanza saa ngapi na
utaishia saa ngapi ili mtahiniwa anapofanya mtihani ajue anatakiwa kujibu mtihani
huo kwa muda maalumu. Pia mtihani unapokuwa unaonesha muda wa kuanza na muda wa
kumaliza unamsaidia mtahiniwa kugawa muda huo wakati wa kujibu maswali ili
kuendana na muda uliopangwa (TET,2002).
Pia uzingatie
kupima makazi ya juu na makazi ya chini ya utambuzi, mwalimu unapo andaa au
kutunga mtihani lazima uweke maswali yatakayo wapima watahiniwa katika makazi
ya juu ya utambuzi na maswali yatakayo wapima makazi ya chini ya utambuzi ili
kujua uwezo wao katika kukumbuka mambo waliyo fundishwa. Hivyo mwalimu lazima
uweke maswali ya kuchagua na maswali ya ufahamu ili kupima katika makazi ya juu
na makazi ya chini kwa watahiniwa. Hii ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote yaani wale hodari na walio wazito wanapata
maswali ya kujibu (TET,2002).
vilevile uwe unapima malengo yaliyo kusudiwa, mwalimu
anapo tunga mtihani anakua na malengo ambayo anatarajia kuyapima hivyo mwalimu
unatakiwa kuandaa maswali yatakayo kusaidia kupima stadi zilizo kusudiwa ili
usije ukawa na malengo ya kupima uwezo wa kusoma na kuelewa kwa kujibu maswali
ukajikuta umetoa maswali ya kuchagua au ya kweli au si kweli baada ya kutoa
kifungu cha habali na kuuliza maswali mafupi yatakayo kusaidia kupima stadi ya
kusoma na kuelewa kile walicho soma (TET,2002).
Pia uwe na
maelekezo yaliyo wazi na yanayo eleweka kwa kila swali, mwalimu unapo tunga
mtihani lazima uzingatie suala la kuweka maelezo yanayo tosheleza na yanayo
eleweka kwa kila swali ili kumwezesha mtahiniwa kujua swali hilo linataka nini
ili aweze kujibu kwa usahihi au kama atakuwa ameshindwa kujibu iwe ameshindwa
kutokana na kutokuwa na kumbukumbu juu ya swali hilo na sio kutoeleweka
kutokana na kukosa maelezo yaliyo wazi (TET,2002).
Vitu muhimu vya
kuzingatia kabla ya kufanya mtihani
Kujua wapi mtihani utafanyika, kabla ya kufanya
mtihani lazima ujue mtihani huo utafanyikia wapi ili uweze kujua kwani tendo la
kujua mtihani utafanyikia wapi ni haki ya mtahiniwa. Pia itamsaidia mtahiniwa
kujua mazingira ambayo atakuwa hivyo itamsaidia kufanya maandalizi ili aweze
kuyakabili mazingira ambayo anakwenda kukutana nayo. Pia itampa ujasiri na
kujiamini katika kujibu mtihani (TET,2002).
Pia kujua muda ambao mtihani utafanyika, muda wa
kufanyika mtihani ukifahamika itasaidia mtahiniwa kujiandaa vizuri katika
kujibu mtihani huo pia mtahiniwa atawahi eneo au chumba ambacho mtihani huo
utafanyika ila mtihani usipo julikana muda wa kufanyika itawachanganya
watahiniwa wa mtihani huo kwani wengine wanaweza kuchelewa kuingia chumba cha
mtihani au wengine wakachelewa kumaliza kwakuwa mtihani haunyeshi muda wa
kumaliza kufanya mtihani huo (TET,2002).
Vilevile kuandaa vifaa vinavyo hitajika katika chumba
cha mtihani, kutokana na kujua wapi mtihani utafanyika na kujua muda ambao
mtihani huo utafanyika itamsaidia mtahiniwa kuandaa vifaa vitakavyo saidia
katika kujibu mtihani katika chumba cha mtihani vifaa hivyo ni kama vile; rula,
kalamu ya wino, mkebe ulio timia vifaa, kikokotoo, kifutio na penseli. Hivi ni
vifaa vinavyo kusaidia wakati wa kujibu maswali ya mtihani unapo kua chumba cha
mtihani (TET,2002).
Aidha kusoma maelekezo ya mitihani, kabla ya kujibu
mtihani mtahiniwa unatakiwa kusoma maelekezo ya mtihani huo kwakuwa maelekezo
huwa na vitu ambavyo vinakatazwa hivyo usiposoma unaweza ukafanya mambo tofauti
na mtihani unavyo taka na hatimaye ukafukuzwa ndani ya chumba cha mtihani na
kufeli mtihani. Hivyo katika mtihani maelekezo ni jamba muhimu sana kuzingatia
kwani maelekezo ni sehemu mojawapo ya mtihani yaani ukishindwa kufuata
maelekezo maana yake umeshindwa mtihani (TET,2002)
Pia kusoma maswali yote ili kujua kama kunaswali
limekosewa au la, kabla ya kujibu mtihani unapaswa kusoma maswali yote ili
kujua kaa kuna swali limekosewa ili uweze kutoa taarifa mapema usije ukajibu
kitu ambacho hakipo hivyo unatakiwa kuhusika kisha kama mtihani wako una maswali
yote yaliyo kusudiwa kuwapo katika mtihani huo. Pamoja na haya tuliyo yajadili
tumeona tujadili na vitu vinavyo ambatana na mitihani kama vifuatavyo (TET,
2002)
Umuhimu wa mitihani ni ka vile, kupima ufanisi wa
mitaala ya elimu, kusaidia katika kuchagua wanafunzi wa kuingia kidato cha
kwanza, au kwa darasa la nne kuchaguliwa kuingia darasa la tano, pia inasaidia
kuwa motisha walimu ambao wanafunzi wamefaulu somo lake na walimu ambao
wanafunzi wamefeli somo lake huwa ni changamoto hivyo huwafanya waongeze bidii
katika ufundishaji ili wanafunzi wafaulu (WEU,2005)
Matumizi ya matokeo ya mitihani ni kama ifuatavyo,
hupima na kutahini maendeleo ya wanafunzi katika ngazi fulani ya elimu,
kutathmini ubora wa elimu inayo tolewa, hutumika katika kufanya maamuzi ya
kielimu kama uchaguzi wa wanafunzi kuingia katika ngazi fulani ya elimu au
kujiunga na kozi fulani, hupima na kutathmini ufanisi wa walimu na mitaala na
husaidia kuleta ushindani katika kujifunza (WEU,2005)
Hivyo mtihani unapokuwa na sifa zote zinazotakiwa na
watahiniwa wakizingatia vitu muhimu kabla ya kufanya mtihani watakapo fanya
mtihani huo upimaji utakuwa umefuata vigezo na matokeo yake tunaweza kuyatumia
katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
REJEA
TET
(2002): historia na maendeleo ya elimu
Tanzania: macmillan Aidan, Dar es salaam.
WEU
(1999):moduli ya misingi ya elimu somo la
kwanza: wizara a elimu na utamaduni. Dar es salaam
WEU
(2005):moduli ya upimaji, tathmini na
utafiti wa kielimu, wizara ya elimu na utamaduni. Dar es salaam
TET
(2002): upimaji na utahini wa maendeleo
ya mwanafunzi. macmillan Aidan,
Dar es salaam
REJEA.
WEU, (2005). Moduli ya somo la upimaji na tathmini katika elimu. Dar es salam.
KEH, (2013). Wikipedia. Sw.wikipedia.org Dar es salaam.
REJEA
WEU,
(2005). Moduli ya somo la upimaji na
tathmini katika elimu. Dar es salaam
WU, (2014).
Walimu na ualimu. www.jiandae.worldpress.com
Rossi, P.H
& Freeman, H.E (1993). Upimaji na
tathmini. Dar es salaam.