Wengine, hasa madereva, hupenda kutumia vinywaji hivi ili kuondoa uchovu na kuwafanya wasipate usingizi. Hufanya hivyo ili wasisinzie na kusababisha wasababishe ajali. Kwa upande mwingine pia, wapo wanaokunywa vinywaji hivi vya kuongeza nguvu kama starehe au mbadala pale wanapokuwa hawatumii vilevi.
Duniani kote matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu kwa sasa yameongezeka kuliko unavyofikiria. Takwimu zilizotolewa katika utafiti uliochapishwa mwaka 2009 katika jarida la ‘Drug Alcohol Dependence’ toleo la 99(1–3), zinaonyesha kuwa mwaka 2006 pekee, takribani aina mpya 500 za vinywaji hivi ziliingizwa sokoni.
Ongezeko hili kubwa la vinywaji vya kuongeza nguvu, linazua mashaka kwa wataalamu wa afya kuhusu usalama wa afya ya jamii. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, matumizi makubwa ya vinywaji hivi yanaambatana na madhara ya afya ya mwili na akili kwa watumiaji.
Watanzania wengi hasa vijana kwa sasa wanapendelea kutumia vinywaji hivi kwa wingi. Kwa sasa soko la vinywaji baridi limejaa vinywaji vya kuongeza nguvu. Ni jambo la kawaida kuona watu wazima na watoto wakinywa vinywaji hivi safarini, katika sherehe mbalimbali na katika kumbi za starehe. Vinywaji hivi huuzwa kwa wingi katika maduka makubwa (Super markets), maduka madogo, hotelini na katika migahawa.
Miongoni wa watumiaji wakubwa wa vinywaji hivi ni wanamichezo na madreva hasa wa magari yanayofanya safari za masafa marefu, ambao wanaamini kuwa kwa kutumia vinywaji hivi huongeza nguvu za mwili, kasi ya vitendo, umakini na kupunguza uwezekano wa kupata usingizi. Watu wengi wanapotumia vinywaji hivi pia huvichanganya na pombe.
Vinywaji vya kuongeza nguvu, visivyo na kilevi, kisayansi vinaelezwa vina kiasi kikubwa cha kafeini, vitamini pamoja na kemikali za taurine, glucuronolactone. Wakati mwingine pia huongezewa dawa aina ya guarana pamoja na mitishamba aina ya ginseng kwa lengo la kusisimua akili na kuongeza nguvu za mwili. Mtafiti wa madhara ya dawa za kulevya wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Stephen Nsimba anasema kwamba vinywaji hivi vina kiasi kikubwa cha kafeini ambayo ni dawa inayosisimua ubongo na kwa kuvichanganya na pombe athari zake kwenye mfumo wa fahamu za mwili huongezeka.
“Baada ya kuchanganya vinywaji hivi, kafeini katika vinywaji vya kuongeza nguvu, hupunguza athari za kilevi na kumfanya mtumiaji asibaini haraka kuwa amekunywa kiasi kikubwa cha kilevi. Hili ni jambo la hatari” anaonya Dk Nsimba.
Habari mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya watengenezaji wa vinywaji hivi huweka kiasi kikubwa cha kemikali kuliko inavyotazamiwa katika hali ya kawaida na hawaonyeshi katika lebo ama karatasi ya maelezo inayobandikwa kwenye kifungashio. April mwaka jana, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TDFA) ilikamata makopo 1,526 ya vinywaji vya kuongeza nguvu katika soko la Tanzania ambavyo vilikuwa havikidhi viwango vya ubora na usalama kwa matumizi ya binadamu.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mkurugezi wa TFDA, Hiiti Sillo aliyoitoa Aprili 3, 2014 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Matokeo ya utafiti mmoja yaliyowasilishwa katika mkutano wa mwaka 2013 wa Chama cha Afya ya Moyo cha Marekani (American Heart Association) uliofanyika katika mji wa New Orleans, ilibainika kuwa kunywa kopo moja hadi matatu ya vinywaji vya kuongeza nguvu, kunaweza kusababisha moyo udunde bila mpangilio na kuongeza shinikizo la damu.
Utafiti huo unaongeza kusema kuwa, hali kama hiyo inaweza kusababisha kifo cha ghafla au magonjwa sugu kama vile shinikizo la damu, kisukari na kiharusi kwa baadhi ya watu.
Dk Gordon F. Tomaselli, ambaye ni msemaji wa American Heart Association (AHA) anasema: “Ingawa jambo hili linaoneka kama dogo lakini linaweza kusababisha madhara makubwa kwa baadhi ya watu. Wale walio na magonjwa ya moyo au historia ya magonjwa hayo katika familia zao, ni lazima wajiepushe na utumiaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu.”
Baadhi ya watu wanaokuwa hawana habari kuwa wana magonjwa ya moyo hasa pale, ugonjwa unapokuwa katika hatua za mwanzo, wanaweza kuhatarisha maisha yao kwa kunywa vinywaji vya kuongeza nguvu ambavyo vina kiasi kikubwa cha kafeini.
Kiasi kikubwa cha kafeini kinaweza kusababisha shinikizo la damu, kuweweseka, kukosa usingizi, maumivu ya kichwa na degedege. Baadhi ya watafiti wanabainisha kuwa vinywaji hivi pia vinaweza kusababisha ugonjwa wa kisukari.
Utafiti wa Dk. D.C. Greenwood na wenzake uliochapishwa katika jarida lijulikanalo kama Europian Journal of Epidemiology, toleo la 25(4) la mwaka 2010, unabainisha kuwa matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu wakati wa ujauzito, unaweza kusababisha mimba kuharibika, kuzaa mtoto mfu au kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu.
Kina mama wanaonyonyesha pia wanapotumia vinywaji hivi huwasababishia watoto wao matatizo ya kiakili ikiwa ni pamoja na kulia kupita kiasi. Vijana wanaotumia vinywaji hivi, pia wanakabiliwa na hatari ya kutumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya, tumbaku na ulevi wa pombe wa kupindukia.
Utafiti wa hivi karibuni nao umebaini kuwa vijana na watoto wanaotumia vinywaji hivi hupata athari za kiakili kiasi kwamba uwezo wao wa kujifunza na kutambua mambo unaathirika.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa T. Van Batenburg-Eddes na wenzake uliochapishwa katika jarida la Front Psychology toleo la 5, mwaka 2014. Utafiti wa jeshi la Marekana uliochapishwa mwaka jana unabainisha kuwa, wanajeshi wengi wanaokunywa vinywaji vya kuongeza nguvu wanakabiliwa na hatari ya kujiua.
Utafiti huo unaongeza kusema kuwa wanajeshi wanaochanganya vinywaji vya kuongeza nguvu pamoja na pombe wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kujiua. Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa H.B. Mash na wenzake uliochapishwa katika jarida la Social Psychiatry and Psychiatric Epidemiology, toleo la 49(9).
Kutokana na athari za vinywaji hivi kiafya, jamii inashauriwa kupunguza au kujiepusha na matumizi yake.
Ni busara pia mamlaka za kiserikali na kidini zinazohusika na usalama wa afya ya watoto zikasaidia kuielimisha jamii kwamba watoto na vijana walio chini ya miaka 18 wasitumie vinywaji hivi. Ni vyema vinywaji kama hivi vikapigwa marufuku.