Utangulizi
Maharage ni moja kati ya mazao ya jamii ya mikunde. Jamii ya mikunde hujumuisha mazao kama kunde, mbaazi, karanga, soya, choroko na maharage yenyewe. Maharage pamoja na mazao mengine ya jamii yake yana sifa moja kuu, yana vinundu kwenye mizizi yake. Vinundu hivyo vinawahifadhi bakteria maalum (nitrogen fixing bacteria) wanaotengeneza nitrogen. Hii ndio sababu ya kwanini mimea jamii hii inafahamika kwa sifa ya kujitengenezea mbolea yake.
Zao la maharage linapendwa na wakulima wengi kwa sababu kwanza linachukua mda mfupi kukomaa, pili halina gharama kubwa katika uzalishaji wake na tatu lina bei nzuri sana sokoni karibu nyakati zote hata wakati wa mavuno (yaani msimu wake). Mkulima anaweza kulima maharage kwa matumizi ya chakula tu nyumbani kwake au kwa biashara reja reja au kwa jumla.
Urahisi wa kulima maharage na faida zake lukuki ni kivutio kwa watu wengi sana lakini bila kufuata muongozo wa kitaalam ni ndoto kwa mkulima kupata mavuno anayotarajia.
Mazingira na Hali Ya Hewa
Hustawi vizuri maeneo yenye mwinuko wa mita 800 hadi 2000 kutoka usawa wa bahari. Joto linalofaa kwa ukuaji wa maharage ni wastani wa jotoridi la nyuzi joto 20 mpaka 29 ingawa katika baadhi ya maeneo huanzia nyuzijoto 15.
Kwa Tanzania maharage hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Kigoma, Arusha, Morogoro, Kagera, Kilimanjaro, Tanga, Ruvuma na Rukwa.
Udongo Unaofaa
Maharage hustawi vizuri katika udongo wa tifutifu au tifutifu yenye mchanganyiko na kichanga wenye rutba na usiotuamisha maji. Chachu ya udongo inafaa iwe ni kati ya 5.5 - 7.0 kwa kipimo vya pH ingawa maharage yanaweza kuvumilia hata pH ya 4.5.
Mbegu Bora za Maharage
Mbegu bora ni zile zilizofanyiwa tafiti na taasisi zinazotambulika kisheria na zikapitishwa na Kamati ya Taifa ya Mbegu (The National seed committee). Miongoni mwa mbegu bora za maharage zilizozalishwa katika nyakati tofauti tofauti na sasa zinatumiwa na wakulima ni pamoja na Uyole, Zawadi, Lyamungu 85 & 90, Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90, Bilfa na Canadian wonder. Mbali na hizi zipo pia mbegu zinazozalishwa na wakulima wenyewe lakini chini ya usimamizi wa TOSCI (Tanzania Official Seed Certification Institute) kwa ajili ya matumizi ya mbegu wao wenyewe au kuuza kwa wakulima wenzao ndani ya eneo husika.
Wakati wa kupanda
Katika mikoa ya mashariki: mwezi Machi/Aprili
Mikoa ya kanda ya ziwa: Agosti/Septemba na Januari/Februari
Nyanda za juu kusini: Novemba/Desemba, Februari/ Machi
Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike wakati muafaka kwa eneo husika kutegemeana na upatikanaji wa maji ya kutosha (mvua). Pia maamuzi ya wakati wa kupanda maharage yazingatie kuwa wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani. Maji mengi yaliyotuama siyo mazuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza. Ukame nao haufai kwani unaweza kukausha mazao na kukuletea hasara. Hivyo kabla ya kupanda haikisha una chanzo cha uhakika cha maji.
Maandalizi ya mbegu
Mbegu za maharage zipo za aina nyingi sana, kuna mbegu bora ambazo zimefanyiwa utafiti na kupitishwa na zipo pia zinazozalishwa na wakulima (mbegu za msimu uliopita zilizohifadhiwa kwa ajili ya msimu ujao). Ni juu yako kufanya maamuzi ya mbegu unayoitaka lakini ni vizuri kutumia mbegu bora kwa kuwa zinazaa sana na zingine zinastahimili magonjwa mbalimbali. Mbegu bora za maharage zinapatikana ASA (Agricultural Seed Agency), makao makuu yao ni Morogoro lakini wana matawi Arusha, Mwanza na Njombe. Lakini pia unaweza kuuliza kwenye maduka ya mbegu za mazao yaliyo karibu yako.
Kiasi cha mbegu
Ili kupanda ekari moja unahitaji kuwa na kiasi cha kilo 30 mpaka 40 za maharage. Hii ni sawasawa na Kg 80 hadi 90 za maharage kwa hekta. Unaweza kupanda mbegu moja au mbili katika kila shimo, lakini mbegu mbili ni bora zaidi na huleta mavuno mengi kwa eneo.
Nafasi ya upandaji
Ikiwa utapanda mbegu mbili za maharage katika kila shimo tumia nafasi ya sm 50 kwa sm 20 yaani sm 50 kati ya mstari na mstari na sm 20 kati ya mmea na mmea (shimo na shimo). Ukipanda mbegu moja katika kila shimo tumia nafasi ya sm 50 kwa sm 10. Hii ukuletee mimea kati ya 150, 000 na 200, 000 katika hekta moja.
Kudhibiti magugu
Maharage yanahitaji palizi mbili za jembe la mkono. Katika palizi ya kwanza ondoa magugu shambani mara tu yanapoonekana lakini hili lifanyike angalau wiki ya pili tangu maharage kuota. Palilia tena kabla maharage hayajachanua. Kupalilia maharage yanayochanua au yenye matunda kunasababisha kupukutisha maua na/au matunda. Lakini pia unaweza kutumia madawa ya kuuwa magugu kama vile Galex 500EC, Stomp 500EC, Dual gold, sateca, n.k. Njia zote zinafaa.
Mahitaji ya Mbolea
Maharage hayahitaji nitrogen kwa wingi kwa sababu mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen. Hata ivo maharage yanahitaji phosphorus kwa ajili ya kuboresha mizizi na potassium kwa ajili ya kuuandaa mmea kwa ajili ya kutoa maua mengi na kuzaa matunda bora.
Ikiwa shamba lililimwa zao ambalo liliwekwa mbolea kama vile Urea au CAN basi huna haja ya kuweka tena mbolea za nitrogen badala yake unaweza kuweka TSP au DAP Kg 60 kwa hekta wakati wa kupanda. Au mbolea ya minjingu (Minjingu Rock Phosphate) Kg 250 kwa hekta moja wakati wa kupanda.
Kama shamba limechoka sana au halikuwekwa mbolea za nitrogen msimu uliopita basi tumia NPK katika uwiano wa 5:10:10 kiasi cha Kg 30 kwa hekta, nayo iwekwe wakati wa kupanda. Mbolea zote ziwekwe sentimita tano hadi 10 kutoka kwenye shina/shimo la mmea na urefu wa sentimita 3 hadi 5 kwenda chini.
Pia unaweza kutumia mbolea ya zizi/samadi (tani 5 - 10 kwa hekta) au mbolea ya kijani (green manure, tani 5 kwa hekta). Mwaga/tawanya samadi kwenye shamba lote halafu ichangane vizuri na udongo kwa kulima kwa plau (la tractor au ng’ombe). Maana yake ni kwamba mwaga samadi kabla ya kulima shamba lako kwa trekta/ng’ombe.
Mbolea ya kijani inapatikana kwa kusafisha shamba halafu ukaliacha mpaka majani/magugu yakaota kisha ukalilima kwa trekta au ng’ombe (likiwa na magugu hivyo hivyo) lakini kabla hayajatoa mbegu halafu ukapanda. Mbolea ya minjingu inaweza kutumika pamoja na samadi na mbolea ya kijani.
Umwagiliaji
Maharage huhitaji mvua ya kutosha kipindi cha kabla ya uwekaji maua (before flowering) na kipindi cha ukuaji wa vitumba vya maharage (podding). Huhitaji unyevu kidogo kipindi cha kuweka maua (during flowering) na ukavu kipindi cha kukomaa (pod maturation) na kukauka vitumba. Vitumba ni matunda (pods). Ikiwa utatumia njia nyingine yoyote ya umwagiliaji angalia maharage yako yapo katika hatua gani kabla hujapanga ratiba yako ya umwagiliaji (irrigation schedule).
Kilimo mchanganyiko (Intercropping)
Tafiti zinaonesha kuwa mavuno ya maharage yaliyopandwa pekee yake ni makubwa ulinganisha na mavuno ya maharage yaliyochanganywa na mahindi au zao lingine. Hii inatokana na ukweli kwamba tofauti na maharage yaliyochanganywa na mazao mengine, maharage yaliyopandwa peke yake hayana ushindani kwenye chakula, mwanga na nafasi na hivyo kufanya yajitosheleze kimahitaji wakati wote wa ukuaji na hivyo kuleta mavuno mengi.
Hata hivyo ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia. Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage.
Inashauriwa kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous) kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama vile wadudu (nzi weupe wa maharage).
Kukomaa, Kuvuna na kupiga Maharage
Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka kinapokuwa kimefikiwa. Dalili za maharage kukomaa ni pamoja na majani kubadilika rangi na kuwa ya njano na mengine kukauka, na mapodo ya maharage kuanza kutoka kwenye ukijani ulioiva na kuwa kijani iliyopauka hadi njano na hatimaye kaki. Pia unaweza kuthibitisha kwa kumenya mapodo na kujiridhisha maharage yalivyo kwa ndani. Maharage makavu huchukua siku 75 (miezi miwili na nusu) hadi 100 kuwa tayari kwa kuvunwa kutegemeana na aina ya maharage. Ikiwa katika kila mimea 10 ya maharage saba au zaidi imekomaa basi maharage yako yapo tayari kuvuna.
Maharage yamekusanywa kwenye turubai tayari kwa kupiga |
Wakati wa kuvuna kwa kawaida mmea wote wa maharage hung’olewa na kukusanywa kwenye vilundo na baadaye vilundo vyote hukusanywa sehemu moja juani ili maharage yakauke kabla ya kupiga. Siku mbili baada ya maharage kung’olewa huwa yamekauka kiasi cha kutosha hivyo unaweza kupiga. Baada ya kupiga pepeta maharage yako ili utenganishe mbegu safi na takataka. Kumbuka kuwa ni lazima utandike turubai chini kabla ya kukusanya maharage yako na kupiga.
Kupepeta maharage baada ya kupiga |
Namna ya kuhifadhi Maharage
Ikiwa utahitaji kuyahifadhi yaanike juani kwa siku kadhaa kuhakikisha yamekauka na hayana unyevu unaoweza kusababisha yapate fangasi. Yahifadhi kwenye magunia na kama yatakaa kwa muda mrefu bila kuuzwa/kuliwa basi hakikisha unayahifadhi kwa kutumia dawa za kuulia wadudu kama vile Shumba, Actellic Dust au Malathion.
Au Tumia mifuko maalum ya kuhifadhia nafaka au chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na endelea kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha kuyafunika tena. Hakikisha kuwa ghara au chombo unachotumia kuhifadhia maharage ni kisafi.