Mr. KASKAZI

Pozi la furaha, Tarehe muhimu. NMB Mtwara Manispaa.

Mr. KASKAZI na walimu wengine

Nikiwa nawasilisha maarifa tuliyochambua kama kazi ya kundi. Najivunia kuwa Mwalimu.

Walimu tuwasaidie wanafunzi kadiri ya uwezo wetu

Mwaka 2016, Wanafunzi wa Shuke ya Msingi MCHOLI II.

SHULE YA SEKONDARI LUKULEDI

Kitovu cha maarifa yangu. Nimepitia magumu mengi na sasa ni muda wa mafanikio. salam na heshima kubwa kwa walimu.

MR. SHAFII KASIM (SHAKA)

Mwalimu ni rafiki wa kweli. Jamii ielewe haipaswi kuchukia walimu.

Showing posts with label KILIMO. Show all posts
Showing posts with label KILIMO. Show all posts

FIKIA LENGO LA MAISHA YAKO KWA UJUZI ULIONAO


Iwe unaomba kazi, unajaribu kufanya biashara au hata unatongoza mtu, vitu vyote hivi vinahitaji ujuzi wa kushawishi. Ujuzi wa kushawishi utakusaidia sana kupata vitu unavyotamani kuwa navyo.

Ukikaa na kufikiria utagundua kuwa kila siku tunajaribu kuuza kitu. Inaweza isiwe bidhaa bali mara nyingine inaweza ikawa ni mawazo yetu (mfano wakati unajadiliana na wenzako kuhusu mpira). Mara nyingine tunajaribu kumshawishi yule machinga apunguze bei ya madela yake ili ununue. Hapa pia unatumia ujuzi wa kushawishi kwa sababu unatumia ushawishi kufikisha lengo lako.

Ujuzi wa kushawishi utafungua milango iliyokua imefungwa, utaleta msaada kwako wakati ukiwa na shida na utakupa mafanikio ambayo hukutegemea. Anza leo kujenga ujuzi huu na utakusaidia maisha yako yote. Unajengaje? Kama ilivyo katika kujifunza kuendesha baiskeli, ushawishi unajifunza kwa kujaribu tena na tena. Anzisha biashara na utajifunza kushawishi wateja, nenda sokoni ukashawishi wauzaji wakupunguzie bei katika manunuzi yako na pia kama lengo lako ni kumpata mwenza, jaribu kutongoza watu wengi uwezavyo na utajenga ujuzi wa kushawishi katika eneo hilo.

Bidii na juhudi zako zitakuwezesha kufanikiwa kupata ujuzi wa kushawishi. Ukiwa na ujuzi huu basi utakua unakaribia zaidi mafanikio katika sekta yoyote ya maisha yako.

KILIMO CHA KARANGA KINAWEZA KUKUTOA

Karanga ni mojawapo ya mazao yanayotoa mafuta. Katika Tanzania zao hili hustawi zaid katika mikoa ya Kusini Mashariki, Dodoma na Morogoro,Mikoa ya Kanda ya ziwa Shinyanga na Geita, pia Kilimanjaro, Mbeya na Mikoa mingine ya Tanzania. Pamoja na kutoa mafuta vile vile zao hutumika kwa njia nyingine mbali mbali,




Nazo ni pamoja na: 

1. Chakula cha wanyama (Mashudu na majani)
2. Kurutubisha ardhi
3. Chakula cha binadamu (Confectionary)

 Kwa ujumla zao hili hutumika na wakulima kama zao la biashara.


HALI YA HEWA
Karanga hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye miinuko chini ya mita 1500, toka usawa wa bahari katika Tanzania, na hustawi zaidi katika maeneo ambayo yanapata mvua za wastani wa mm 750 hadi mm 1200 kwa mwaka.
Vile vile karanga hustawi vizuri kwenye udongo wa kichanga, inashauriwa kutopanda karanga kwenye udongo mzito (mfinyanzi) hii ni kutokana na sababu kwamba, karanga hazistawi kwenye sehemu zinazo simama maji, na udongo mzito huleta hasara wakati wa uvunaji.




AINA ZA KARANGA
Kuna aina kuu tano bora za karanga ambazo zimetolewa kwa wakulima hapa nchini.


a. Red Mwitunde 
Ilitolewa kwa wakulima miaka ya 1950.
Mbegu za muda mrefu (Virginia Spreading bunches).
Huchukua muda wa siku 120 -140 toka kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kutoa kilo1000 kwa hekta. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi nyekundu.


b. Nyota
Ilitolewa mwaka 1983.
Mbegu ya muda mfupi ( Spanish Errect Banch).
Huchukua siku 90-100 tangu kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kuzaa wastani wa kilo1500 kwa hekta. Mbegu zake ni ndogo, na zina rangi ya udongo (Tan).
Aina hii ya mbegu zina tabia ya kuanza kuota tena shambani mara tu zikiisha komaa, hivyo ni muhimu kuzivuna mapema zikisha komaa.


c. Johari:
Ilitolewa mwaka 1985.
Mbegu ya muda wa kati (Virginia Spreading Bunches).
Huchukua siku 110 - 120 toka kupanga kuvuna. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi ya udongo (Tan). Ina uwezo wa kutoa wastani wa kilo 1000 kwa hekta moja.




d. Pendo: . 
Ilitolewa mwaka 1998.
Mbegu ya muda mfupi ( Spanish Errect Banch). Huchukua siku 90-100 tangu kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kuzaa wastani wa kilo 1500 kwa hekta. Maganda yake ni laini na mbegu zake ni kubwa, na zina rangi ya udongo (Tan). Kama Nyota, aina hii ya mbegu ina tabia ya kuanza kuota tena shambani mara tu zikisha komaa, hivyo ni muhimu kuzivuna mapema zikisha komaa.


e. Sawia:
Ilitolewa mwaka 1998.
Mbegu ya muda wa kati (Virginia Spreading Bunches).
Huchukua siku 110 - 120 toka kupanga kuvuna. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi ya udongo (Tan). Ina uwezo wa kutoa wastani wa kilo 1000 kwa hekta moja.

Pamoja na mbegu zilizotajwa, kuna aina nyingine nyingi za kienyeji (local varieties) zinazotumiwa na wakulima katika sehemu mbali mbali.


UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Shamba litayarishwe vizuri kuwezesha udongo kupenyesha maji na mizizi kirahisi. Karanga hupandwa kwenye matuta au sensa (shamba tambarare).


UTAYARISHAJI WA MBEGU
Karanga ambazo zinakusudiwa kwa mbegu zitunzwe na maganda yake bila kubanguliwa. Zibanguliwe karibu na msimu wa kupanda na kuchaguliwa. Baada ya kuchaguliwa zitiwe dawa, aina ya Fernasan D, Katika uwiano wa gramu 28 za dawa kwa kila kilo 10 za mbegu safi.




WAKATI WA UPANDAJI
Uamuzi wa kuchagua wakati mzuri wa kupanda niule utakaoliwezesha zao hilo kukomaa wakati wa mvua za mwisho. Kuchelewa kupanda, hupunguza mavuno. Ni muhimu kuchagua aina ya mbegu ambazo uvunaji wake unafanana na mazingiza ya eneo hilo kihali ya hewa.

Kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, karanga za muda wa kati na mrefu (Johari, Red Mwitunde) zipandwe kuanzia katikati, hadi mwishoni mwa mwezi Desemba. Karanga za muda mfupi (Spanish na Valencia) zipandwe kuanzia mwishoni mwa mwezi Desemba hadi katikati ya mwezi Januari.
Kwa mikoa ya Tanga, Morogoro na sehemu za mkoa wa Dodoma, karanga zipandwe mapema mwanzo wa mvua ndefu. (Februari/March).


NAFASI KATI YA MIMEA
Inashauriwa kupanda karanga katika mistari. Nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 15, kwa karanga zinazotambaa (Virginia Spreading types). Kama karanga zinapandwa kwenye matuta ya sentimita 90, zipandwe mistari miwili, kila tuta. Kwa nafasi hii kiasi cha kil 60-75 za mbegu hutumika kwa hekta moja.

Kwa karanga zilizopo kwenye kundi la Spanish/Valencia (zisizotambaa), nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 10. Endapo karanga zimepandwa kwenye matuta ya sentimita 90, panda mistari miwili , inayofanya nafasi sawa na sentimita50 kwa sentimita 10. Kiasi cha kilo 80-100 za mbegu hutumika kwa hekta moja kwa kutumia nafasi hii.Kwa ina zote za mbegu, panda mbegu moja safi, katika kila shimo.


MBOLEA
Kufuatana na majaribio yaliyofanyika imeonekana kuwa karanga hustawi vizuri chini ya viwango vidogo vya phosphorus (TSP, SSP). Vile vile katika sehemu nyingine, karanga zimefanya vizuri kwa kutumia samadi. Ubadilishaji wa mazao (Crop Rotation) husaidia kutunza rutuba, hivyo kupunguza kiasi cha mbolea kinachotumika.Karanga zinaweza kulimwa baada ya mahindi, ili kutumia masalia ya mbolea.


UPALILIAJI
Karanga zipaliliwe zikiwa changa. Shamba lililotayarishwa vizuri na kuondolewa magugu ya muda mrefu (Perrenial weeds) linaweza kupalliwa mara moja, kwa sababu karanga hukua haraka, na zinaweza kushindana na magugu. Baada ya kutoa maua, karanga zisipaliliwe, hii inaweza kuharibu 'pegs', hatimaye kupunguza mavuno.


MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU:

1. MAGONJWA



(i) Ugonjwa wa kuoza (Aflatoxin)

Katika hali ya unyevu mwingi vimelea viitwavyo Aspegilus flavus huota ndani ya maganda na kushambulia mbegu za karanga. Vimelea hivyo hutoa kemikali ambayo ni sumu.


KUZUIA

  • Hakikisha kuwa karanga haziharibiwi wakati wa kuchimba.
  • Hakikisha karanga zinakaushwa vizuri (Unyevu wa 10%) kabla ya kuzitunza zitumike kama mbegu
  • Karanga za kupanda zitiwe dawa aina ya Fernasan-D.


(ii) Ugonjwa wa Madoa na Kutu: (Cercospora Leaf Spots and Rust)
Magonjwa haya husababisha madoa ya rangi ya kikahawia hadi meusi kwenye majani.

Vimelea vinavyosababisha magonjwa haya viko vya aina tatu:


(a) Cersospora arachidicola. Husababisha Early Leaf Spot.
(b) Phaeoisariopsis personata. Husababisha Late Leaf spot.

Ugonjwa wa Early Leaf Spot hutangulia kuonekana, lakini magonjwa yote mawili yanaweza kujitokeza shambani kuanzia wiki 3-5 baada ya karanga kupandwa.

(c) Puccinia arachidis. Husababisha ugonjwa wa Kutu.

Kuzuia:
  • Kupanda mapema.
  • Kuondoa maotea ya karanga wakati wa kiangazi.
  • Tumia dawa aina ya Chlorothalonil (Daconil 2787)


Dawa huwekwa kiasi cha kilo l.6 katika lita 800 za maji kwa hekta moja, kila baada ya siku saba, kwa majuma machache kuanzaia maratu dalili za ugonjwa zinapoonekana.

Uchunguzi juu ya aina zinazostahimili magonjwa haya bado unaendele kufanywa kwenye kituo cha utafiti wa kilimo Naliendele.


(iii) Ugonjwa wa Rosette (Rosette virus disease)
Ugonjwa huu huambukizwa na wadudu waitwao "Mafuta" Aphids (Aphis craccivora). Mimea ambayo imeshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa, na inakuwa na madoa ya njano.
Ugonjwa wa Rosette (Ukoma)

Kuzuia:
  • Kupanda mapema
  • Panda karanga zako shambani katika nafasi za karibu karibu.
  • Palilia na toa maotea shambani mwako.


(iv) Ugonjwa wa maganda matupu (Empty pods or pops)
Karanga zilizoshambaliwa na ugonjwa huu, huwa lazina mbegu (maganda matupu). Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa madini ya Calcium (chokaa) kwenye udongo

Kuzuia:
Tumia Calcium katika hali ya Gypsum (Ca SO4) kwenye mimea au weka Chokaa (lime - CaO) kwenye udongo kabla ya kupanda. Ugonjwa huu uko kwenye mikoa ya kusini mwa Tanzania (Lindi, Mtwara na Ruvuma) na hushambulia sana karanga za muda mrefu kama vile Red Mwitunde.
Majaribio hapa Tanzaniia hayajathibitisha kuweka chokaa (Liming) kuwa ni jibu sahihi la kupambana na ugonjwa huu, lakini ili kupunguza, kupanda mapema ni muhimu.


2. WADUDU WAHARIBIFU
(i) Mafuta Aphids au "Mafuta" (Aphis cracivora)
Hushambulia karanga kila msimu, lakini athari yao kubwa ni kueneza ugonjwa wa Rosette. Wakati wa mvua nyingi huoshwa toka kwenye majani, hivyo hawaleti madhara.



Kuzuia:

• Kupanda mapema
• kupanda karanga karibu karibu




(ii) Groundnut hopper: Hilda patruelis
Hufyonza mizizi, "pegs", na karanga changa, hivyo husababisha majani kuwa manjano, kunyauka, na mmea kukauka ungali mchanga. Wadudu hawa hushambulia mazao mengine kama vile maharage, kunde. alizeti na korosho, hivyo kunahitajika mzunguko (rotation) mzuri wa mazao.

Kuzuia:
• Kwenye mashamba makubwa, inashauriwa kutumia dawa aina ya Aldrin au chloropyrifos, kuchanganya kwenye ardhi kabla ya kupanda.
• Kunyunyizia Dimethoate mara tu wadudu wanapoonekana.
• Kutochanganya na zao la korosho au mbaazi kwenye shamba moja na karanga.


(iii) Mchwa.
Kuna aina mbili za mchwa ambao hushambulia na kusababisha uharibifu kwenye zao la karanga.
Aina ya kwanza ni wale ambao hutoboa sehemu ya chini kwenye mzizi, au kutengeneza matundu, na hukaa kwenye mmea wa karanga wakati wote zikiwa shambani.
Aina ya pili ni wale ambao hukata matawi yanayokua au kutambaa. Uharibifu huu huonekana zaidi kwenye shamba jipya. Kuchelewa kuvuna kunaweza kusababisha kupotea kwa mazao mengi, kutokana na kuharibika kwa mizizi, na kusababisha karanga nyingi kubakia shambani wakati wa kuvuna.

Kuzuia:
Mchwa wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa aina ya Alandrin 40% ya unga, kwa kiasi cha kilo 2.5 kwa hekta., Njia rahisi ni kuchanganya dawa na mbolea aina ya Phosphate(TSP au SSP) au mchanga na kumwaga shambani kabla ya kupanda karanga.


(iv) Panya:
Hushambulia sana karanga zinapoanza kuota, na wakati zinapokaribia kuvunwa.

Namna ya Kuzuia panya:
• Tumia dawa za kuua panya
• Mitego
• Kuwachimbua toka aridhini walikojificha.


(v) Ndege
Kama panya, ndege hasa kunguru hushambulia sana karanga kabla hazijaota (mara baada ya kupanda), zinapoanza kuota, zinapokaribia na wakati zimekwisha komaa.

Kuzuia
• Kutumia mitego
• Kuamia
• Kuweka (kutundika/kuning’iniza) mzoga au kunguru mzima shambani.


UBANGUAJI NA UTUNZAJI WA KARANGA
Kubangua karanga ni kazi ngumu. Mtu mmoja anaweza kubangua kiasi cha kilo 12-15 kwa siku. Karanga zilizopo kwenye kundi la Virginia hubangulika kirahisi, kuliko aina yaSpanish au Valencia. Mashine za kubangulia karanga hupatikana hapa nchini, zinarahisisha kazi, lakini tahadhari isipochukuliwa huharibu karanga.

Karanga zinazokusudiwa kutunzwa kwa muda mrefu, zitunzwe na maganda yake kwenye ghala. Ghala iwe kavu, yenye kupitisha hewa, na imara kuzuia wanyama waharibifu kama vile panya.Ubora na uwezo wa karanga kuota huanza kupotea mara baada ya kubanguliwa.

MBINU ZA KUPATA MTAJI KWA AJILI YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI MWINGINE

Watu wengi huwa wanajiuliza ni namna gani wanaweza kupata fedha kwa ajili ya kuanzisha biashara au aina fulani ya ujasiria mali. pamoja na makala mbalimbali zinazokuonesha namna gani uwe kama mjasiriamali hii ya leo ni namna ya kupata mtaji.

1. kuuza sehemu ya mali yako. 
hii ikiwa na maana kuwa, unaweza kuwa na amana ambayo ukiuza unaweza kupata pesa ambayo inaweza kuanzisha mradi utakaokuingizia mara dufu. unaweza kujiuliza mali yako ipi? mfano, nguo zako, meza, kabati, baiskeli, pikipiki na vingine ambavyo unaweza ukapata pesa ya kuanzisha mradi.

2. zawadi mbalimbali (fedha).
chukulia kuwa umemaliza kozi fulani katika jitihada zako za masomo. katika mahafali yako familia, ndugu, jamaa na marafiki wanakutunza kwa kukupatia kiasi cha fedha. kiasi hiko cha pesa kinatosha kabisa kuwa mtaji katika mbinu zako za ujasiria mali.

3. mshahara kutoka kwa mwajiri wako.
katika kufanya kazi ongeza bidii. mwajiri anapokulipa pesa inatosha kabisa kuwa mtaji katika ujasiriamali unaoukusudia. wakati mwingine watu husema mbinu hii ni kwa watumishi pekee la hasha bali mwajiri hata yule anayekupa shughuli ndogondogo kuzifanya kisha anakupatia pesa kutokana na shughuli hiyo. kusanya kiasi hiko kwa kurudia rudia mpaka unajikuta ukifikia lengo la kiasi cha mtaji wako unaoukusudia.

4. mikopo.
niseme tu kuwa siku hizi taasisi za fedha zimekua nyingi. mikopo katika mbinu hii inaweza kuwa moja kati ya sehemu zifuatazo.  
  • benki mfano; NMB, NBC, CRDB, BENKI YA POSTA 
  • taasisi za fedha. MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII (NSSF, LAPF, PSPF, PPF), FAIDIKA, ABC, MABOTO NK. 
  • vikundi vya akiba (vikoba) VIKUNDI VYA KUWEKA NA KUKOPA 
  • kwa ndugu na jamaa. KWA MJOMBA, BABA NA MAMA NK.

5. bahati nasibu.
pia bahati nasibu nazo zimekua nyingi na watu pia wamekua wakishinda kwa kishindo. zipo nyingi ila hapa nitataja chache tu. mbet, tatumzuka, biko nk 

hizo ni baadhi ya mbinu za kupata mtaji. kama unakumbuka na nyingine komenti hapo chini; G+, twitter, facebook au comment

KAMA MNATAKA MALI MTAIPATA SHAMBANI


Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali,
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,
Wakataka na kauli iwafae maishani.

Akatamka mgonjwa, ninaumwa kwelikweli,
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali,
Roho naona yachinjwa, kifo kimenikabili,
Semeni niseme nini, kiwafae maishani.

Yakawatoka kinywani, maneno yenye akili,

Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali,
Urithi tunatamani, mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani

Baba aliye kufani, akajibu lile swali,

Ninakufa maskini, baba yenu sina hali,
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,

Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
Akili zetu nyembamba, hazijajua methali,
Kama tunataka mali, tutapataje shambani?

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,

Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,

Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili,

Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,

Tangu zile za mibuni, hadi zitupazo wali,
Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali,

Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,
Wote wakashangilia, wakakumbuka kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakanunua na ng'ombe, majike kwa mafahali,

wakapata na vikombe, mashine na baiskeli,
Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,
Wakakiweka kibao, wakaandika kauli,
Kama mnataka mali, mtaipata shambani.


 

KILIMO CHA STRAWBERRY




UTANGULIZI
Zao hili hustawi katika joto la wastani, na hukua kwa haraka zaidi na uzalishaji kuongezeka linapolimwa kisasa, hasa katika nyumba maalumu ya kuzalishia mimea yaani green house.
Katika Tanzania zao hili linakuwa vizuri mikoa ya Morogoro na Iringa
Zao hili hukua vizuri katika mwinuko wa mita 1,500 kutoka usawa wa bahari.
Endapo unahitaji kuzalisha strawberry katika maeneo ya bondeni itakulazimu kuwa na maji kwa wingi kwa ajili ya umwagiliaji wa mara kwa mara.
Strawberry inaweza kustawi vizuri kwenye udongo tifutifu wenye rutuba. Zao hili haliwezi kustahimili ukuaji kwenye udongo wenye chachu nyingi, hasa chokaa kwani mizizi yake huoza kwa urahisi.
KUPANDA
Ili kuwa na mazao bora ambayo yatakuwezesha kupata soko la uhakika, bila vipingamizi, inashauriwa kuzalisha kwenye nyumba maalumu ya kuzalishia mazao (green house). Katika kuzalisha strawberry baada ya kujenga green house andaa mabomba ya plastiki ambayo yatawezesha kutoboa matundu kwa urahisi Matundu katika bomba hilo yawe na umbali wa inchi 1.
• Ni vyema matundu hayo yakawa zigzag, ili kuruhusu mimea utakayopanda kukua vizuri bila kuwekeana kivuli.
• Tandika karatasi la nailoni sakafuni ili kuwezesha maji utakayotumia kunyeshea kurudi kwenye bwawa au sehemu ya kuhifadhia.
• Ning’iniza mabomba hayo kwa kutumia waya.
• Jaza kokote, yenye mapande makubwa kiasi.
• Panda miche kwenye kila tundu kwa uangalifu ili mizizi isikatwe na kokoto zinazoshikilia mmea. Kumwagilia Mimea ya strawberry inahitaji maji kwa kiasi kikubwa sana.
Hii inamaanisha kuwa unahitaji kuwa na mfumo mzuri wa umwagiliaji kabla ya kuanza kilimo cha zao hili. Unapaswa kumwagilia mara nne kwa siku, kila baada ya saa nne unapaswa kumwagilia kwa robo saa. Hii itawezesha mimea yote kupata maji ya kutosha.
Endapo strawberry haitapata maji ya kutosha, uzalishaji wake pia utakuwa ni hafifu sana, kwani maua ya Strawberry inapooteshwa kwenye greenhouse hutoa mavuno mengi na yenye ubora. atachanua ipasavyo na hata matunda kukomaa inakuwa ni shida.
MBOLEA
Uzalishaji wa kisasa wa strawberry, unaambatana na ufugaji wa samaki kwenye bwawa ndani ya green house. Mbinu hii husaidia mimea kupata mbolea inayotokana na chakula wanacholishwa samaki kwenye bwawa, kwani maji yanayofugia samaki ndiyo hayo yanayotumika katika mzunguko wa umwagiliaji.
Hii inamaanisha kuwa hakuna mbolea nyingine inayohitajika kwa ajili ya strawberry. Wadudu na magonjwa Endapo strawberry inazalishwa kwenye nyumba maalumu ya mimea, hakuna magonjwa wala wadudu wanaoishambulia.
UZALISHAJI NJE YA GREENHOUSE
Ikiwa mkulima anazalisha strawberry kwenye eneo la wazi, strawberry inaweza kushambuliwa na magonjwa ya ukungu, pamoja na magonjwa yanayosababishwa na virusi.
DAWA
Endapo strawberry itashambuliwa na magonjwa ya ukungu na virusi, nyunyizia dawa za asili kama vile pareto na mwarobaini, na baada ya muda kutakuwa na matokeo mazuri.
KUVUNA
Zao la strawberry, huzaliana na kukomaa kwa haraka sana. Unaweza kuanza kuvuna strawberry baada ya mwezi mmoja tangu kupandwa.
Kila wiki strawberry inakuwa na matunda mapya, na kila tunda likishatokeza huiva kwa haraka, hivyo uvunaji wake ni wa mfululizo.
Ikishafikia hatua hiyo tegemea kuwa na wiki 2 hadi 3 za kuvuna mfululizo. Kwa kuwa matunda ya strawberry ni laini, epuka kushika tunda wakati wa uvunaji ili lisiharibike.
Shika kikonyo cha tunda ili kuvuna kwa usalama. Usiache matunda yaliyoiva shambani kwa muda mrefu kwani yanaweza kusababisha mimea kuoza.
Pia yatapoteza ladha na virutubisho halisi vinavyotakiwa. Virutubisho Strawberry ina kiasi kikubwa cha virutubisho hasa vitamin B, C, K, na E .
Pia yana wingi wa madini ya chumvi. Matunda haya husaidia kuchangamsha mwili na yana kiasi kidogo cha kalori.
MATUMIZI:
 
Matunda ya strawberry yana matumizi mbalimbali kulingana na uhitaji wa mtumiaji, jamii na maeneo. Miongoni mwa matumizi hayo ni pamoja na:
• Kuliwa kama tunda.
• Kutia ladha katika aina mbalimbali za vyakula.
• Kuweka rangi, harufu na nakshi katika vipodozi.
• Kutengeneza marashi n.k.
SOKO:
Soko zuri kulingana na ubora wake. Kwa sasa gramu 500 za strawberry zinauzwa kati ya shilingi 5,000/= hadi 10,000/= za kitanzania.