Namna ya Kulima Nanasi


Utangulizi

Nanasi ni tunda la kitropiki, linapendwa na walaji wengi kwa sababu ya ladha yake tamu na harufu yake nzuri. Tunda hili laweza liwa mara tu baada ya kuvunwa, baada ya kulipika, au kama juisi. Nanasi ni chanzo kizuri cha vitamin A na B, pia inakiwango kingi tu cha vitamin C pamoja na madini kama vile: patasiam, magnesiam, kalsiam, na madini chuma.

Asili ya nanasi inaaminika kuwa ni Brazil na Paraguay huko Amerika ya Kusini. Hapa Tanzania, nanasi hulimwa zaidi maeneo ya Bagamoyo, Kibaha (Pwani), Tanga, Mtwara, Lindi, Geita na Mwanza. Lakini pia maeneo yote ya pwani ya Tanzania yanafaa kwa kilimo cha nanasi.

Hali ya hewa inayofaa kwa ukuaji wa nanasi
Kilimo cha nanasi kinapendelea hali ya hewa ya joto na husitawi vema katika mwinuko kati ya mita 0-1750 kutoka usawa wa bahari. Mwinuko wa mita 1300 hadi 1750 hufaa zaidi kwa uzalishaji wa nanasi kwaajili ya kusindika na mwinuko chini ya hapo hufaa zaidi kwaajili ya ulaji wa moja kwa moja. Mahitaji ya joto ni kati ya nyuzi joto 18°C hadi 35°C.


Udongo unaofaa kwa kilimo cha nanasi
Kwa kilimo cha nanasi chachu (pH) ya udongo inayofaa ni 5.5 hadi 6.0, na hustawi vizuri zaidi katika udongo tifutifu na udongo wenye kichanga usiotuamisha maji. Ingawa nanasi huweza kustawi katika udongo wa aina yoyote ile, udongo wa mfinyanzi haufai kwa kilimo cha nanasi.

Maandalizi ya shamba
Lima shamba kwa trekta, kwa ng’ombe ama kwa jembe la mkono kwa kina cha sentimita 30 hadi 45. Shamba la nanasi unaweza kulilima kwa sesa (flat-bed) au kwa matuta (furrows).

Kwa sesa: chimba mashimo kwa nafasi ya sm.60 kati ya mistari, sm. 30 kati ya miche na sm. 80 kati ya kila mistari miwili. Weka mbolea kianzio katika kila shimo na upande, hakikisha shamba lina unyevu wa kutosha kabla ya kupanda. Weka tani 10 hadi 15 za mbolea ya kuku, weka pia viganja 2 vya mbolea ya zizi katika kila shimo.

Upandaji wa mananasi
Zipo aina mbali mbali za ‘mbegu’ (machipukizi/maotea) lakini yale yanayochipua kutoka ardhini hufaa zaidi na hukomaa mapema. Chagua machipukizi mazuri yenye umri mdogo na yenye kulingana kwa ukubwa. Iweke miche kwenye kivuli kwa siku 3 kabla ya kuipandikiza iweze kutoa mizizi haraka. Pandikiza mwanzoni mwa mvua za masika. Nafasi iwe sm.60 kati ya mistari, sm. 30 kati ya miche na sm. 80 kati ya mistari miwili. Pandikiza miche 50,000 katika hekta moja. Chovya miche kwenye dawa ya Diazinon au Fention kwa muda wa dakika 25 kabla ya kuipandikiza ili kuzuia mashambulizi ya wadudu.

Palizi
Palilia shamba mara kwa mara ili kuhakikisha shamba halina magugu. Katika kilimo cha nanasi magugu hudhibitiwa kwa palizi ya jembe, kung’oa kwa mkono ama matumizi ya viuagugu. Matumizi ya viuagugu hurahisisha zaidi palizi ya nanasi ukizingatia kuwa nanasi huwa na miiba katika ncha za majani yake ambazo huchubua ngozi endapo palizi za jembe zitatumika. Njia nyingine ni matumizi ya matandazo (mulch) ya majani au plastiki (plastic mulch) maalum kuzuia magugu.


shamba-la-mananasi
Shamba la mananasi

Mahitaji ya mbolea ya mananasi
Weka mbolea ya NPK gramu 50 hadi 70 kwa kila mche wakati wa kupanda. Weka tena gramu 85 kwa kila mche baada ya miezi 3 na pia miezi 3 baadae.

Wadudu na Magonjwa yanayosumbua minanasi
Nanasi ni zao lisilosumbuliwa na wadudu ama magonjwa mara nyingi. Hii ni faida kubwa sna kwa wakulima wa nanasi! Hivyo endapo patatokea mashambulizi ya wadudu na magonjwa, ushauri zaidi wa kitaalam utafutwe kukabiliana na tatizo husika. Hakikisha unakagua shamba ili kuzuia wadudu kama wataonekana.

Uvunaji wa mananasi
Nanasi huanza kutoa maua miezi 12 hadi 15 baada ya kupanda kutegemeana na aina ya nanasi au maotea ya mbegu yaliyotumika, muda wa kupanda na joto la mahali husika. Kwa kawaida nanasi hukomaa miezi 5 baada ya kutoa maua, hivyo nanasi huchukua miezi 18 hadi 24 kukomaa/kuiva. Katika kilimo cha nanasi, mimea ikitoa maua kwa nyakati tofauti tofauti itasababisha kuvuna kidogo kidogo na kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo ndio maana ni muhimu kupanda kwa wakati mmoja mbegu zenye umri na ukubwa sawa.

Kwa wanaofanya kilimo cha nanasi kibiashara (commercial pinapples production) hutumia kemikali aina ya Ethrel (@ 100 ppm) mwezi mmoja kabla ya kuanza kutoa maua ili mimea mingi iweze kutoa maua kwa wakati mmoja, angalau 80% ya mimea yote.

Vuna wakati kikonyo cha nanasi kimebadilika rangi kuwa njano ya dhahabu. Kata kikonyo cha nanasi chenye urefu wa sm. 30 kikiwa kimeshikana na nanasi na upunguzie majani ya kichungi chake.

Utunzaji wa mananasi
Hifadhi nanasi katika eneo lenye ubaridi huku kikonyo chake kikielekea juu. Hakikisha unauza nanasi mara tu au siku 2 hadi 3 baada ya kuvuna ili kutunza ubora wake.


mananasi-yaliyovunwa
Mananasi yaliyovunwa