Mambo 5 Yatakayokupa Hamasa Katika Safari Yako Ya Mafanikio


Katika safari ya mafanikio ni rahisi sana kufanikiwa ikiwa ndani yako kila siku unakuwa una hamasa kubwa ya kukusaidia kufikia mafanikio hayo. Mara nyingi hamasa huwa ni kama kichocheo cha kukufanya uzidi kukazana na kuweza kuendelea hadi mwisho kwenye mafanikio yako.

Kwa kawaida hamasa inapokesekana, hapo sasa ndipo mambo huanza kufanyika kivivu na wakati mwingine kukata tamaa huanza kujitokeza. Hivyo, utaona kwamba kuwa na hamasa tena kubwa ikiwa unataka mafanikio ni kitu cha lazima sana, vinginevyo uwe hupendi kufanikiwa.

Utakapokuwa na hamasa hii, suala la kukatishwa tamaa linakuwa sio rahisi sana kwako. Sasa kutokana na umuhimu wa hamasa kwenye mafanikio ni vizuri ikiwa utafanya mambo yatakayokupa hamasa ya kufanikiwa kila siku. Kwa kusoma makala haya, utajua mambo hayo ya msingi kabisa yatakayokupa hamasa. Karibu tujifunze kwa pamoja.


1. Jikumbushe malengo yako kila wakati.

Nguvu kubwa ya kufanikiwa na kupata hamasa utakuwa unaipata ikiwa utakuwa mtu wa kujikumbusha malengo yako kila wakati. Unaweza kujikumbusha malengo yako asubuhi, mchana na hata jioni iwe kwa kuyaandika au kuyasoma. Unapojikumbusha malengo yako kila siku hiyo inakupa hamasa kubwa ya kufanya kitu cha ziada juu ya malengo yako bila kuacha.

2. Fanya kile Unachokipenda.
Mara nyingi kufanya kile unachokipenda ni njia sahihi ya kukufanya kuwa na hamasa wakati wote. Hiyo ni kwa sababu, hata ikitokea kitu hicho hakileti matokeo unayoyataka kwako halitakuwa tatizo kwa sababu ni kitu ambacho unakipenda na kipo kwenye damu. Hivyo, unalazimika sana kufanya lile jambo unalolipenda ili kuwa na hamasa ya mafanikio kila siku.

3. Weka nguvu zako kwenye jambo moja.
Kama kuna jambo umeamua kulifanya weka nguvu na mawazo yako hapo. Acha kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja hayatakusaidia sana. Lakini, unapofanya jambo moja na kuweka nguvu zote hapo kufunga hiyo ni nguvu tosha ya kukupa hamasa, kwani utajifunza mengi sana kutokana na kitu hicho kimoja na itakusadia kukupa hamasa ya kuendelea mbele.


4. Kuwa chanya wakati wote.

Huwa si jambo geni sana kukatishwa tamaa hasa pale tunapokuwa kwenye safari ya mafanikio. Hiyo huwa inatokea kwa sababu watu wengi wako hasi sana.  Sasa ili kuepuka hilo inabidi ujifunze namna unavyopokea taarifa hasi na kutafsiri matukio. Kwa kufanya hivyo itakusaidia kujenga ile hamasa ambayo ipo ndani mwako na idumu kila siku na mwisho wa siku utafanikiwa.

5. Acha kujilinganisha na wengine.
Kati ya sumu kubwa inayoweza ikakufanya ukakosa hamasa ya kuendeea mbele kimafanikio ni pamoja na kujilinganisha na wengine. Siku zote kimbia mbio zako mwenyewe. Ukijilinganisha sana, mwisho utaanza kujikosoa na kujiona hufai. Hivyo unataka kuwa na hamasa kubwa kila siku, kuwa wewe kama wewe, kwa hilo litakusidia sana.

Kwa kujua mambo hayo, yatakusaidia sana kukujengea hamasa kila siku. Fanyia kazi mambo hayo ili yawe silaha ya kukusaidia kukupa hamasa na kufanikiwa pia.
Ansante kwa kusoma makala haya na tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.