Katika kipindi cha hivi karibuni ambapo watu wengi wamekua wakijaribu kuingia katika biashara, kumekua na watu wengi sana wakiuliza swali hilo hapo juu. Ukiingia mtandaoni napo utakuta wengi wanauliza swali hilohilo. Na watu wengine hutoa majibu kama “nunua bodaboda”, “fanya kilimo”, “fungua kiwanda cha matofali” kisha huanza kutoa mchanganuo wa mtaji utakaohitaji, mapato utayopata, jinsi utavyopata faida kubwa na kupanua biashara yako na baada ya miaka mitano utavyokuwa umepata hela nyingi sana kiasi unaelekea kuwa tajiri.
Kwa kuwa michanganuo kama hiyo huwa inavutia sana, basi watu wengi hujitosa katika biashara bila kufanya uchunguzi wa ndani zaidi. Michanguo haisemagi ufanye nini dereva wako wa bajaji anapoumwa kwa mwezi mzima, wala haisemi ufanye nini mteja wako unaemdai mamilioni anapokuzungusha kukulipa. Haikuambii nini cha kufanya unapojikuta wewe ni mmoja wa wakulima 30 mnaojaribu kuiuzia Nakumatt maembe kwa wakati mmoja wala haisemi ufanye nini kuku wako ambao uliambiwa “hawashiki magonjwa kirahisi”, wanapouumwa mara kwa mara. Na ndipo unapokuta mambo kama haya yanapotokea, mtu hukata tamaa na kuamua kuachana na biashara. Ni moja ya sababu kubwa biashara 9 kati ya 10 hufa ndani ya mwaka mmoja.
Ukweli ni kwamba, wengi wetu tunapata “kichaa” tunapoona jinsi michanganuo inavyoonesha pesa nyingi. Baada ya kuona jinsi bwawa la samaki litavyotuletea milioni 80 baada ya miaka 3 tunaanza kufikiria gari mpya tutakayonunua au tutavyoandaa sherehe ya kufa mtu tutaporudi kijijini kwetu Sengerema. Tunashindwa kuuliza kuhusu changamoto au kutafuta wale walio katika biashara hiyo tayari na wamefanikiwa ili watupe mawaidha na mwongozo ili nasi tufanye vizuri. Lakini swali la muhimu zaidi ambalo hatujiulizi ni nini tufanye ili kuhakikisha wateja wanavutiwa kufanya nasi biashara na sio competitors. Ni nini cha thamani tunaweza kuwapa wateja wetu kilicho zaidi ya kinachotolewa na kampuni nyingine?
THAMANI. VALUE. Wengi tunadhani biashara ni kuhusu pesa. La hasha, biashara ni kuhusu THAMANI. Ni thamani gani unatoa kwa wateja wako? Je thamani hiyo ni ya kutosha kumfanya mtu kuwa mteja wako wa mara kwa mara? Je, thamani gani unatoa kwa wafanyakazi wako? Unadhani thamani hiyo inatosha kuwafanya wawe na furaha, wachapakazi na wasikuibie?
Mohammed Dewji anajua kati ya ishu muhimu kuhusiana na bidhaa ndogondogo kwa watanzania ni bei na upatikanaji. Ndio maana bidhaa zake ni za bei ya chini kuliko nyinginezo lakini pia ni rahisi kupatikana. Hiyo ndio thamani anayotupatia. Na sasa tayari ni tajiri namba moja Tanzania. Pia kuna kijana mmoja kule Zanzibar alikuwa na bodaboda moja miaka kadhaa iliyopita. Sasa ana bodaboda 6, na gari nyingine za biashara. Kijana huyu hulipia matibabu ya madereva wake wanapopata ajali, huwapa zawadi wanapoleta mahesabu kwa wakati, na huwapa asilimia ya mauzo ya bodaboda au gari pale anapoliuza ili kuwapa moyo madereva wake watunze vyombo hivyo vizuri ili viuzwe kwa bei kubwa. Kijana huyu anatambua thamani anayoweza kuwapa madereva wake ni kuonesha kuwajali na motisha nzuri. Hajawahi kupata shida kubwa na wafanyakazi wake.
Hiyo ni mifano michache ya jinsi unavyoweza kufanikiwa kwa kutoa thamani kwa wale unaojihusisha nao katika biashara yako. Hili liwe wazo lako la kwanza unapoamka na liwe la mwisho kabla ya kulala. Utapofanya jambo hili kuwa namba moja katika biashara yako, basi ile sherehe kule Sengerema utafanya tu bila shaka. Watu hawapendi kutoatoa hela zao, ila ukiwapa kitu cha thamani kiasi kwamba wanasahau wanakilipia, utakuwa tajiri mkubwa sana.