Iwe unaomba kazi, unajaribu kufanya biashara au hata unatongoza mtu, vitu vyote hivi vinahitaji ujuzi wa kushawishi. Ujuzi wa kushawishi utakusaidia sana kupata vitu unavyotamani kuwa navyo.
Ukikaa na kufikiria utagundua kuwa kila siku tunajaribu kuuza kitu. Inaweza isiwe bidhaa bali mara nyingine inaweza ikawa ni mawazo yetu (mfano wakati unajadiliana na wenzako kuhusu mpira). Mara nyingine tunajaribu kumshawishi yule machinga apunguze bei ya madela yake ili ununue. Hapa pia unatumia ujuzi wa kushawishi kwa sababu unatumia ushawishi kufikisha lengo lako.
Ujuzi wa kushawishi utafungua milango iliyokua imefungwa, utaleta msaada kwako wakati ukiwa na shida na utakupa mafanikio ambayo hukutegemea. Anza leo kujenga ujuzi huu na utakusaidia maisha yako yote. Unajengaje? Kama ilivyo katika kujifunza kuendesha baiskeli, ushawishi unajifunza kwa kujaribu tena na tena. Anzisha biashara na utajifunza kushawishi wateja, nenda sokoni ukashawishi wauzaji wakupunguzie bei katika manunuzi yako na pia kama lengo lako ni kumpata mwenza, jaribu kutongoza watu wengi uwezavyo na utajenga ujuzi wa kushawishi katika eneo hilo.
Bidii na juhudi zako zitakuwezesha kufanikiwa kupata ujuzi wa kushawishi. Ukiwa na ujuzi huu basi utakua unakaribia zaidi mafanikio katika sekta yoyote ya maisha yako.